Watu waliotawanywa na mchafuko Sudan wakivuka mpaka kwenda Sudan Kusini. (Maktaba)
11 Oktoba 2024 Wahamiaji na Wakimbizi
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR limetangaza leo Oktoba 11 kwamba Sudan Kusini sasa inawahifadhi zaidi ya wakimbizi nusu milioni katika maeneo 30 nchini humo, hasa katika kambi za wakimbizi za Maban, Jamjang, Wedweil na Gorom.
Ikichochewa na mzozo unaoendelea nchini Sudan, idadi hii imeongezeka karibu maradufu tangu mwaka 2023, ikionesha kuongezeka kwa athari za mgogoro katika eneo lote. Sudan Kusini imepokea idadi kubwa ya pili ya watu wanaokimbia Sudan, na zaidi ya watu 810,000 wamewasili tangu Aprili 2023.
"Idadi ya wakimbizi nchini Sudan Kusini imeongezeka karibia maradufu katika kipindi cha chini ya miezi 18 na tunatarajia hali mbaya zaidi itakuja. Mzozo wa Sudan unaikumba Sudan Kusini zaidi kuliko nchi nyingine yoyote katika eneo hilo na unaongeza changamoto kubwa ambazo taifa hilo linakabili," Amesema Marie-Helene Verney, Mwakilishi wa UNHCR nchini Sudan Kusini na kuongeza kwamba "UNHCR na watendaji wengine wa kibinadamu wamekuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na misaada ya kibinadamu na sasa wanatoa wito kwa wengine kujiunga na juhudi za kusaidia Sudan Kusini kuunganisha mamia kwa maelfu waliofika. ”
“Ni wazi, hata hivyo, kwamba suluhu pekee ni kumalizika kwa mzozo nchini Sudan. Sudan Kusini inakabiliwa na mshtuko na haiwezi kuendelea kustahimili mateso mengi hivyo,” ameongeza Verney.
Zaidi ya nusu ya wakimbizi wote nchini Sudan Kusini kwa sasa wanahifadhiwa katika Kaunti ya Maban na wakimbizi wengine 135,000 wanaishi katika eneo la Utawala la Ruweng. Hata hivyo, idadi inayoongezeka ya watu wanaowasili hivi karibuni wanachagua kuishi katika maeneo ya mijini, wakileta yote mawili, fursa na changamoto ndani ya uchumi na jamii.
Mwaka 2024 umeleta changamoto ambazo hazijawahi kushuhudiwa kwa Sudan Kusini
Mgogoro unaoendelea nchini Sudan umetatiza pakubwa njia za usambazaji na uuzaji wa mafuta nje ya nchi, kuinua mfumuko wa bei na kudhoofisha zaidi uchumi. Bei za bidhaa muhimu ikiwa ni pamoja na chakula zimepanda sana, na hivyo kupunguza rasilimali zinazopatikana katika jumuiya zinazowakaribisha, na kuifanya iwe changamoto kubwa kujumuisha wawasiliaji wapya.
Hata hivyo, UNHCR pamoja na Kamisheni ya Masuala ya Wakimbizi ya Sudan Kusini chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, na wadau wengine wanaendelea kusaidia wahamiaji wapya na jamii zinazowapokea. “Mbali na kukidhi mahitaji ya haraka ya watu ikiwa ni pamoja na maji, makazi na matibabu, pia tunahamasisha suluhu za muda mrefu kwa wakimbizi na wanaotafuta hifadhi, ikijumuisha upatikanaji wa vitambulisho, fursa za kujikimu na kujumuishwa katika mifumo ya kitaifa kama vile afya na elimu. Usaidizi mkubwa zaidi wa kimataifa kwa ajili ya ufumbuzi wa kudumu kama vile makazi mapya pia ni muhimu.” Inaeleza UNHCR.
Wakati ufadhili kwa Sudan Kusini ukiendelea kuwa wa ukarimu, rasilimali za kukidhi mahitaji ya watu kikamilifu bado ziko chini sana. Kufikia Oktoba 2024, shughuli za UNHCR nchini zilifadhiliwa kwa asilimia 47 pekee. Tunaendelea kuomba msaada zaidi wa wafadhili kwa majibu.
Kabla ya Aprili 2023, Sudan Kusini ilikuwa tayari nyumbani kwa wakimbizi 275,000, wengi wao wakitoka Sudan na walikuwa wamewasili zaidi ya muongo mmoja uliopita. Idadi hii inakuja wakati takriban Wasudan Kusini milioni 2 wamekimbia makazi yao, na robo tatu ya watu wote wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.