Wafahamu viongozi watano wa upinzani Afrika walioshtakiwa kwa uhaini hivi karibuni

Mashitaka ya uhaini yanayomkabili kiongozi wa cham kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema Tundu Lissu yamekitikisa chama hicho na kuishitua dunia. Siku ya Alhamis tarehe 10 Aprili, karibu magazeti yote makubwa ya dunia yalikuwa na habari ya kesi hiyo kubwa kabisa ya Lissu.
Mwenyekiti wa zamani wa Chadema, Freema Mbowe, ni kiongozi wa upinzani wa hivi karibuni kushitakiwa na kukaa ndani kwa takribani miezi 8 kati ya mwaka 2021-2022. Lakini yeye alishitakiwa kwa kosa tofauti la ugaidi, ambalo halina dhamana. Hata hivyo kesi yake ilifutwa mwezi Machi, 2022, baada ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, DPP kusema hana nia ya kuendelea na kesi.
Tundu Lissu na kesi hii ya uhaini anaweza kuwa ndiye mwanasiasa wa kwanza wa upinzani nchini Tanzania kushitakiwa kwa kosa hilo lisilo na dhamana.
Lakini kwa barani Afrika, anaungana na wanasiasa wengine wapatao sita, ambao serikali zao ziliwatia matatani kwa mashitaka kama hayo hayo ya uhaini.
Kizza Besigye

Chanzo cha picha, Getty Images
Pasi na shaka, mwanasiasa huyu wa upinzani kutoka nchini Uganda ndiye kinara wa mashitaka haya ya uhaini baada ya kushitakiwa mara mbili ndani ya kipindi cha miaka chini ya 15. Mara ya kwanza Besigye alishitakiwa kwa uhaini mnamo mwaka 2006 mashitaka yaliyoambatana na ugaidi.
Miaka kumi baadae (2016) Besigye alishitakiwa tena kwa kosa hili baada ya kujiapisha kuwa rais kwa kuamini kwamba ushindi aliopewa mshindani wake Rais Yoweri Museveni haukuwa wa haki.
Mwishoni mwa mwaka 2024, Besigye alishitakiwa tena kwa uhaini baada ya kuwa ametekwa akiwa jijini Nairobi nchini Kenya na kudaiwa kusuka mipango ya kununua na kupanga kuingiza silaha nchini Uganda kwa nia ya kupindua serikali ya Rais Museveni.
Mwanasiasa huyu anayeaminiwa kuwa ndiye mwanasiasa wa upinzani aliyekamatwa mara nyingi kuliko yeyotye yule duniani bado anasota jela akisubiria hatma ya kesi yake.
Robert Kyagulanyi aka Bobi Wine

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni nchini Uganda humo humo pia anapatikana mwanasiasa Robert Kyagulanyi, al maaruf Bobi Wine, kutoka chama cha upinzani aliyekamatwa na kushitakiwa kwa makosa ya uhaini chini ya miaka kumi iliyopita. Mnamo mwezi Agosti 2018, Bobi Wine alishitakiwa kwa uhaini pamoja na watu wengine 33, wengi wao wanasiasa baada ya msafara wa Rais Yoweri Museveni kushambuliwa na mawe.
Mahakama ilisema Bobi Wine na wenzake walikuwa na mpango wa kumdhuru rais wa nchi hiyo.
Hakainde Hichilema

Chanzo cha picha, Getty Images
Upande wa kusini mwa Tanzania tunakutana na rais wa sasa wa Zambia Hakainde Hichilema alishitakiwa kwa kosa la uhaini. Hichilema alipewa mashtaka haya baada ya kugoma kuupisha msafara wa rais wa wakati ule Edgar Lungu uliomkuta njiani.
Hii ni kwasababu, Hichelema hakuwa anamtambua Lungu kama rais halali wa nchi yao, baada ya kupoteza kwa kura chache sana katika uchaguzi uliopita. Hichelema alisema Lungu na chama chake waliiba kura.
Miaka minne kamili tangu kuachiliwa huru kwa mashitaka haya (aliachiwa huru tarehe 16 Agosti 2017), Hichelema alitangazwa rais wa Zambia tarehe 16 Agosti 2021.
"Msiwe na wasiwasi, mtakuwa sawa tu. Hata msijali, hamtapigwa mabomu ya machozi" alisema Hichilema katika hotuba yake ya kukubali ushindi, huku ikiaminika kwamba ujumbe huu aliukusudia kwa mtangulizi wake Lungu na serikali yake waliomnyanyasa kisiasa.
Ernest Bai Koroma

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa zamani wa Sierra Leone pia amewahi kukumbwa na madhila haya. Ilikuwa ni Januari mwaka jana tu ambapo mamlaka nchini humo ilimkuta Koroma na kosa la uhaini baada ya kumuhusisha na jaribio la kutaka kumpindua rais wa nchini hiyo.
Mashtaka haya byaliibuka baada ya tukio la uvamizi wa kambi ya jeshi, na kufuatiwa na uvamizi wa magereza uliowaachia huru wafungwa takribani 2000. Mamlaka nchini humo zilihusisha matukio haya mawili na jaribio la kupindua serikali.
Viongozi wa jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi walijaribu kufanya makubaliano na Sierra Leone kuona kama watamuondolea mashitaka hayo Koroma, kwa sharti kwamba Koroma ahamie uhamishoni nchini Nigeria.
Hata kama makubaliano haya hayakufikiwa rasmi, mnamo mwezi Januari 2024, Koroma aliruhusiwa na mahakama kwenda Nigeria kwa sababu za matibabu, lakini hata hivyo hakuna taarifa za uhakika ikiwa amerudi nchini Sierra Leone ama lah
Ousmane Sonko

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiongozi huyu kijana alishitakiwa kwa uhaini na kuchochea machafuko nchini Senegal. Ni kiongozi anayejulikana kupendwa na vijana wengi ambapo mashtaka yake ya awali yahusuyo rushwa yaliibua maandamano makubwa nchini humo na hata kusababisha vifo. Mashitaka haya yaliendelea hadi Desemba 2023 miezi kadhaa kabla ya uchaguzi, ambapo mwezi March 2024 ambapo mwanafunzi wake wa siasa Bassirou Diomaye Faye aliposhinda urais na kumchagua Sonko kuwa Waziri Mkuu.
Hata Faye mwenyewe aliingia madarakani akiwa bado ana vumbi vumbi la jela. Baada ya kuachiwa kutoka gerezani tarehe 14 Machi 2024, chini ya siku ishirini baadae, tarehe 2 Aprili, Faye aliapishwa kuwa rais wa Senegal.
Ni wazi kwamba mashitaka haya ya uhaini si mapya barani Afrika, hasa kwa viongozi na wanasiasa wengine wa vyama vya upinzani. Hata hivyo, wanasheria na watetezi wa haki za binadamu mara nyingi wameyaunganisha na visa vya kisiasa wanavyofanyiwa wapinzani kukwamisha kuving'oa madarakani vyama tawala.
"Huwezi kuyatenganisha mashitaka haya na siasa. Alikuwa anatoa elimu kwa wanachama wa Chadema, lakini wameigeuza kuwa mashitaka ya uhaini" Rugemeleza Nshala aliliambia shirika la habari la Reuters