Hakuna afya bora bila afya ya akili – Guterres

3 months ago 33

Katika ujumbe wake siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema kwa kuzingatia takwimu hizo, hakuna jamii au eneo ambalo liko salama huku akisema, kujiua kunasalia kuwa sababu kuu ya kifo miongoni mwa vijana na mamilioni wanaendelea kutatizwa na afya ya akili kimya kimya.

Ni kwa kuzingatia hilo anasema, Siku ya Afya ya Akili Duniani mwaka huu inajikita katika afya ya akili pahala pa kazi.

“Asilimia 60 ya watu walio na umri wa zaidi ya miaka 15 wanatumia muda wao mwingi wakiwa pahala pa kazi. Maeneo haya ni mahlai ambapo ni zaidi ya pahala pa kazi,” anasema Guterres.

Kufanyia kazi nyumbani kunaibua changamoto ya afya ya akili

Anaongeza kuwa mahali pa kazi palipo salama na penye afya panaweza kumpatia mfu fursa ya kutambua lengo lake, kupata mtandao na utulivu, ilhali mazingira ya kazi kandamizi au yenye vurugu yanaweza kuwa na madhara makubwa kwenye afya ya akili kwa wafanyakazi walioko eneo hilo.

Guterres anaongeza kuwa tangu janga la coronavirus">COVID-19 lifungue milango ya mbinu mpya ya kufanyia kazi mbali na ofisini, mipaka kati ya majukumu ya nyumbani na ofisini yanazidi kutoweka na kuibua changamoto kubwa zaidi ya kulinda afya ya akili ya wafanyakazi.

Kazi ni muhimu kama ilivyo afya ya akili

Kazi ni muhimu kwa ustawi wa kila mtu, lakini pia afya ya mtu ni muhimu kwa ajili ya kazi inayofanwa.

Pindi waajiri wanaposaka suluhu ya hatari za afya ya akili kwa mfanyakazi, wanaongeza motisho, wanapunguza utoro kazini na kuongeza ushiriki wa mwajiriwa katika kuchagiza uchumi,” amesema Guterres.

Ni kwa mantiki hiyo anasema “kila mtu, pahala pa kazi na kwingineko, anapaswa kuwa na ufahamu na rasilimali za kupatia kipaumbele afya ya akili, na kupata huduma za afya ya akili bila kunyanyapaliwa na bila vikwazo.

Sasa Guterres anakumbusha kuwa katika siku hii ya Afya ya Akili duniani, “hebu na tukumbuke kuwa hakuna afya bila afya ya akili. Tuazimie kujenga mazingira ya kazi salama ambamo kwamo watu wanaweza kustawi."

WHO na ILO wanataka hatua zichukuliwe kulinda afya ya akili kwa wafanyakazi wanaofanyia kazi majumbani

WHO na ILO wanataka hatua zichukuliwe kulinda afya ya akili kwa wafanyakazi wanaofanyia kazi majumbani

Waajiri waweke mazingira ya kustawishi watumishi wote

Naye Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus kupitia mtandao wa X, zamani Twitter amesema “wakati huu ambapo wengi wetu ni sehemu ya nguvukazi, nusu ya idadi ya watu wote duniani, hii ina maana kwamba mamilioni ya watu wanaathiriwa vibaya kila siku.”

Amesema msongo wa mawazo na kiwewe peke yao hugharimu uchumi wa dunia dola trilioni 1 kila mwaka, na kiwango hicho kinaweza kuwa kikubwa zaidi kutokana na madhara ya COVID-19, mizozo na janga la tabianchi.

Dkt. Tedros amesema licha ya changamoto hizo, bado uwekezaji kwenye afya ya akili ni kidogo, na watu wengi bado wanakabiliwa na unyanyapaa na kubaguliwa.

Ametaja mazingira yasiyo rafiki pahala pa kazi pamoja na uonevu, unyanyasaji na ubaguzi wa rangi na mashinikizo vinaweza kudhuru afya ya akili.

Dkt. Tedros ameunga mkono kauli ya Guterres ya kutaka maeneo ya kazi yawe saidizi badala ya kuwa chochezi. Na zaidi ya yote, waajiri wabaini vihatarishi na vichochezi vinavyoharibu afya ya akili. Pili mameneja wapatiwe stadi za kutambua viashiria hivyo na kuchukua hatua; na Tatu, kuweka mazingira ambamo kwamo watumishi wote wakiwemo wenye changamoto za afya ya akili waweze kustawi.

Source : UN Habari

SHARE THIS POST