HADITHI: Bomu Mkononi - 8

3 months ago 72

By  Faki Faki

Mwananchi Communications Limited

“WANAJUA kuoga ni asubuhi na jioni na kubadili nguo ni pale wanapotaka kutoka. Wakirudi nyumbani wako ovyo,” nikaongezea chumvi.

“Hawajui kwamba mapenzi yanahusisha pia umaridadi. Wewe unaweza kumpenda mwanaume kwa umaridadi wake tu. Na hivyo hivyo mwanaume anaweza kukupenda wewe kwa umaridadi wako tu. Kwa hiyo mwanamke ni kujijali, usipojijali unaweza kuiweka ndoa yako shakani.”

“Ni kweli,” nikamkubalia kungwi.

“Mume wako anakutana na wasichana warembo kibao lakini anawafumbia macho, anasema naenda kwa mke wangu. Lakini akifika kwako anakukuta uko ovyo, kwa kweli hatakuthamini.”

“Ni kweli.”

“Zingatia sana suala la usafi wa mwili wako, mavazi yako na hata nyumba yako. Ukifanya hivyo utaweza kudumisha ndoa yako.”

Baada ya hapo mwenzangu akawa kimya. Nikahisi alikuwa ameshalala. Kwa vile kila mmoja alikuwa ameelekea upande wake niliamini hivyo tu kuwa alikuwa ameshalala.

Mimi niliendelea kubaki macho nikiwaza. Yale maneno aliyokuwa akinieleza yalikuwa yakipita akilini mwangu. Nikawa nayafanyia uchambuzi wa kina na kuamini kuwa yalikuwa maneno yenye maana ambayo msichana anayetarajia kuolewa kwa mara ya kwanza alitakiwa aelezwe.

Hapo ndipo nilipoona umuhimu wa makungwi. Niliamini kuwa kulikuwa na mengi ambayo ningeyapata kutoka kwa mwanamke huyo.

Baadaye nilipata usingizi lakini haukuwa usingizi niliozoea kuupata nikiwa chumbani kwangu. Nililala kwa wasiwasi sana.

Asubuhi kungwi wangu ndiye aliyeniamsha. Ilikuwa saa kumi na mbili asubuhi.

“Jifundishe kuamka mapema ili uweze kumhudumia mumeo vizuri. Sio mume ameamka, wewe bado umelala. Atahudumiwa na nani?” Kungwi wangu aliniambia.

Sikumjibu kitu. Nikaamka. Alinitoa uani akanipeleka maliwatoni. Nilipiga mswaki nikaoga kisha akanirudisha chumbani.

“Utachemsha chai kwenye jiko la Mchina, mimi ninakwenda kutafuta vitafunio,” akaniambia na kunionesha jiko pamoja na birika.

“Sawa.”

“Utachota maji kwenye ndoo nyekundu. Kopo la majani ya chai, iliki, mdalasini na tangawizi hili hapa.”

Alinionyesha kopo hilo kabla ya kutoka mle chumbani.

Alipotoka nikaanza kushughulika. Nilitia maji kwenye birika kisha nikawasha jiko na kuibandika birika kwenye jiko la Mchina. Nikakaa kwenye kochi kusubiri maji yamchemke.

Wakati birika inaanza kuvuma kuonyesha kuwa maji yalikuwa yanachemka nikatia iliki, mdalasini ambao ulikuwa umeshasagwa pamoja na tangawizi.

Maji yalipozidi kuchemka nikatia majani ya chai kisha nikategua ile birika.

Kungwi wangu aliporudi alinipa chupa ya chai nikatia ile chai.

“Nizime jiko?” Nikamuuliza.

“Zima, halina kazi tena kwa sasa,” akaniambia.

Nikazima jiko na kusimama hapo hapo ili kama kuna kitu kingine aniagize.

“Utapenda kunywa chai muda huu?” Akaniuliza.

“Mimi mpaka kwenye saa mbili au tatu ndio nakunywa chai.”

“Basi tutasubiri hadi muda huo. Nimekuchukulia chapati na vitumbua.”

“Vinatosha.”

“Basi njoo tukae.’

Nikaenda kuketi naye.

 “Nakusisitizia tena ukiwa kwa mumeo jitahidi kuamka mapema kabla ya mumeo kuamka ili uweze kumuandalia mahitaji yake, usipende aamke yeye wewe bado umelala. Kama kutakuwa na kitu anataka atamuuliza nani?” Kungwi wangu akaniambia.

“Nikishaolewa nitakuwa naamka mapema kabla ya mume wangu”

“Lazima kutakuwa na kazi za asubuhi kama vile kuosha vyombo mlivyotumia jana usiku, kufanya usafi wa nyumba yako, kumtayarishia chai mume wako na kadhalika. Wanaume wengine hawawahi kunywa chai majumbani mwao kwa sababu ya majukumu yao lakini wengine wanakunywa majumbani.

“Kama mume wako atakuwa ni mmojawao inabidi umtayarishie chai na vitafunio, vile akitoka kuoga tu akute chai ipo tayari. Kama mtakuwa mnashindana kulala utakuwa umeacha jukumu lako, utakuwa sio mke mwema.” Kungwi wangu akanisisitizia.

“Nitazingatia yote hayo,” nikamwambia.

“Lakini haiishii hapo. Mume wako anapokwenda kazini, baada ya wewe kumaliza majukumu yako ya nyumbani unamuandalia mlo wa mchana, akirudi kazini akute chakula. Kuna waume wengine wanaenda wenyewe masokoni hasa waume wa Kipwani. Lakini walio wengi huwaachia wake zao kwenda masokoni. Umenielewa?”

“Nimekuelewa.”

“Kama mume wako amekuachia jukumu hilo, asubuhi akienda kazini unaenda sokoni, unanunua mahitaji yako ya mchana kutwa. Unahakikisha katika pesa uliyopewa kuna visenti unavibakisha kidogo kwa ajili ya akiba yako. Hivi vinakuwa ni siri yako.

“Wakati mwingine mume wako hana pesa, hivi visenti unavyoweka vinaweza kuwasaidia. Jaribu kuwa muaminifu kwake, kuwa mkweli na jaribu kuwa karibu naye sana kiushauri, kujua matatizo yake na kujua kinachomsibu.”

Wakati kungwi wangu akinipa semina, mimi nilikuwa nikitingisha kichwa changu kama ishara ya kumkubalia.

“Unapokuwa karibu na mume wako na unapokuwa unampa ushauri mzuri, si tu atakuwa anakutegemea bali pia utajua mengi kutoka kwake. Ni vizuri kwa mwanamke kujua yaliyomo ndani ya moyo wa mume wako.”

Niliendelea kutingisha kichwa changu kama ishara ya kumuelewa kungwi wangu.

Ilipofika saa mbili na nusu kungwi wangu aliniambia.

“Andaa chai tunywe.”

Nikanyanyuka kwenye kochi na kwenda kuandaa chai. Nilichukua vikombe viwili nikaviweka kwenye sinia, nikaweka vitafunio kisha nikaweka sukari na kumimina chai.

Wakati tunakunywa chai, mazungumzo yalikuwa yakiendelea.

“Kujenga unyumba ni kazi. Ukiwa legelege ndoa inaweza kukushinda. Inatakiwa ujizatiti sana. Mimi sipendi uolewe leo, keshokutwa tukutane mitaani uniambie nimeachwa. Inatakiwa ujiulize wale wanaodumu katika ndoa zao wana nini na wale wanaoachwa wana nini?” Kungwi aliniambia.

“Bila shaka jibu utalipata kuwa wale wanaodumu katika ndoa zao wamejizatiti na wale walioachwa walikuwa legelege. Ukiwa legelege hata upepo utakuondoa mahali pako.” Kungwi aliendelea kuniambia.

“Pale nilipokwambia ni vyema uwe karibu sana na mume wako ulinielwa vizuri?” Safari hii akanipa swali.

“Nilikuelewa,” nikamjibu nikiamini kuwa nilikuwa nimemuelewa vizuri.

“Umenielewaje?” Akaniuliza tena.

“Nimekulewa kwamba ninatakiwa niwe karibu na mume wangu kimazungumzo, kiushauri na pia kujua matatizo yake.”

“Hukukosea lakini kuna zaidi ya hapo. Kuna kitu kimoja ambacho mume wako hawezi kukipata kwa mwingine isipokuwa ni kwako tu na akikipata kwingine kitakuwa ni haramu. Unakijua?”

Nikatikisa kichwa.

“Labda uniambie.”

“Tendo la ndoa. Linaitwa tendo kwa sababu ni kubwa kwa maana yake. Na linaitwa tendo la ndoa kwa sababu ndio sababu ya msingi ya kuweko kwa ndoa na pia ndio sababu ya msingi wewe umeletwa kwangu.”

Nikamkubalia kungwi wangu kwa kichwa.

“Tendo hilo ndio uti wa ndoa yako, likikosekana ndoa inaweza kuvunjika,” aliniambia kisha akaniuliza.

“Unanikubalia?”

“Ndio nakukubalia.”

“Kama unanikubalia, keshokutwa mume wako anakwambia geuka huku unamwambia nimechoka, kweli wewe unalinda ndoa yako?”

Nikacheka kisha nikatikisa kichwa.

“Hapo nitakuwa silindi ndoa yangu,” nikamjibu.

“Huku kwetu Pwani vazi la khanga linaheshimiwa sana, unajua ni kwanini?’

“Sijui.”

“Mbali ya kuchukuliwa kama vazi muhimu la mwanamke pia ni vazi ambalo linatumika kutoa ujumbe, sema watu wa siku hizi hawalijui hilo. Zamani tukinunua khanga tunaangalia maneno yaliyoandikwa kwenye khanga ile.

“Haya maneno yanasaidia sana kutoa hisia za mwanamke badala ya kutumia mdomo. Kwa mfano kuna mpangaji mwenzako amekuudhi, badala ya kugombana naye unamvalia khanga yenye maneno ya kumpa ujumbe utakaomgusa.”

Hapo nikaangua kicheko.

“Hivyo ndivyo mlivyokuwa mkifanya zamani?” Nikamuuliza.

“Haswa! Si hapo tu. Khanga pia ilitumika kumtolea ujumbe mume wako. Sasa tunarudi kule kule kwenye mada yetu ya tendo la ndoa. Mwenyewe umeshapanga kwamba leo utamfurahisha mume wako, ukishaoga jioni unamvalia khanga yenye ujumbe mahususi kumjulisha kwamba leo kutakuwa na kazi! Si lazima umwambie kwa maneno.

“Na yeye akishasoma ule ujumbe ameshajua kilichokusudiwa. Kama ambavyo wewe umejiandaa na yeye anajiandaa. Cheko na bashasha zinaanza mapema.”

Wakati kungwi akiendelea kunieleza mimi nilikuwa nikicheka tu.

“Mishi unacheka. Mpe raha mume wako. Usimbanie!” Akanisisitizia.

“Nitampa,” nikamjibu.

“Wewe ndiye halali yake, huko kwingine ni haramu. Sasa mzuie mume wako asiende kula haramu.”

Inaendelea...

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST