HADITHI: Bomu Mkononi - 19

1 month ago 19

By  Faki Faki

Mwananchi Communications Limited

Haraka nikajibu: “Wazazi wangu wameshakufa.”

“Wazazi wako wote wawili wamekufa?” Sheikh akaniuliza tena ili apate uhakika.

“Baba na mama wameshakufa.”

“Huna ndugu wengine kama vile kaka?”

“Nilizaliwa peke yangu.”

“Sasa walii wako atakuwa nani?”

“Walii ni nani?” Nikamuuliza.

“Walii ni baba atakayekutolea idhini nikuozeshe.”

“Nitajitolea idhini mwenyewe.”

“Kwani ulishawahi kuolewa chuo cha kwanza?”

Nikatikisa kichwa haraka.

“Hapana, sijawahi kuolewa.”

“Itabidi upate walii. Huwezi kujiidhinisha mwenyewe.”

“Sasa nitampata wapi mimi?”

“Basi mimi nitakuwa walii wako kama utanikubali na pia ndiye nitakayewaozesha. Wewe utakuwa kama mwanangu.”

“Sawa.”

Sheikh akamtazama Mustafa.

“Mimi nitakuwa walii wake wa kumsimamia, ndoa ni lazima walii. Halafu mimi nitawaozesha,” akamwambia.

“Sawa.” Mustafa akamjibu.

Baada ya hapo sheikh akaniambia kuwa kutoka muda ule ninatakiwa kukaa chumbani kama mwari na nivae nguo za sitara na nijitande mtandio kama bi harusi kwani saa chache baadaye atatufungisha ndoa.

Niliambiwa kuwa ndoa hiyo itafungwa msikitini lakini mimi nitabaki nyumbani. Baada ya ndoa ndio Mustafa angekuja kunipa mkono.

Ilikuwa kweli. Ilipofika saa mbili usiku ndoa ikafanyika. Nyumbani nilikuwa mimi na ndugu wachache wa Mustafa waliokuwa wakiishi Dar.

 Baada ya ndoa kufungwa msikitini, mume wangu wa pili Mustafa na sheikh aliyetufungisha ndoa pamoja na watu wachache walikuja nyumbani. Kutokana na udanganyifu nilioufanya kwa kweli niliona aibu. Sikuweza hata kuinua uso wangu kutazama watu.

Jinsi nilivyokuwa nimejiinamia, watu waliokuwa hapo nyumbani walidhani ni mambo ya harusi, kumbe nilikuwa na langu lililonitia fadhaa.

Nilikuwa nimeketi chumbani juu ya kitanda. Watu walipoingia mle ndani wakimsindikiza Mustafa, Sheikh alimwambia Mustafa anipe mkono.

Mustafa akanifunua mtandio niliokuwa nimefunikwa usoni kisha akanipa mkono. Mustafa akiwa ameshikilia mkono wangu, Sheikh alituombea dua ndefu na kisha kutupa wasia wa ndoa.

“Mmeoana kwa wema, nawaomba muishi kwa wema vile vile. Mpendane, mzae watoto wenu waume kwa wake. Na pale mtakapokuwa hamna budi kuachana, muachane kwa wema si kwa ugomvi na uhasama. Mmenisikia vizuri?’

“Tumekusikia Sheikh” Mimi na Mustafa tulijibu kwa pamoja lakini sauti yangu haikutoka. Nikaona nikubali kwa kichwa.

“Tayari mmeshakuwa mke na mume, sisi tunawaacha muendelee na furaha yenu.” Sheikh akatuaga na kuondoka na mashahidi wake.

Kukabaki watu wa karibu tu mle chumbani. Watu hao walikuwa ni wa upande wa Mustafa. Hakukuwa na mtu hata mmoja wa upande wangu. Picha zilipigwa. Zilianza kupigwa tangu watu hao wanaingia mle chumbani.

Watu mbalimbali walikuja kupiga picha na sisi. Baada ya zoezi hilo la kupiga picha kumalizika, tuliitwa mezani kwa ajili ya chakula. Tukatoka mimi na Mustafa na dada yake tuliyekuwa naye, tukaenda kula chakula pamoja na wageni wengine wachache.

Baada ya chakula tukaenda sebuleni kupiga stori. Watu waliokuwa wamehudhuria hapo nyumbani walianza kuondoka mmoja mmoja. Dada yake Mustafa ndiye aliyeondoka mwisho. Tukabaki peke yetu.

Tulipojiona tupo peke yetu tukaingia chumbani. Si unajua usiku wa kwanza wa wana ndoa unakuwaje. Hivyo ndivyo ulivyokuwa kwetu sisi.

Hata hivyo wakati wote sikuwa nikionesha furaha ya kweli. Nilikuwa na hofu na wasiwasi kutokna na ile hatua niliyochukua yakuolewa kwa mara ya pili.

Nilikuwa nikijiuliza endapo Musa atakuja kugundua kuwa nimeolewa tena wakati nikiwa mke wake atachukua hatua gani? Au Mustafa akija kugundua kuwa nilimfanyia utapeli atanitanya nini?

Nilijua kuwa watu hao wanaweza kunishitaki kwa ulaghai wangu lakini bado nilijipa moyo kuwa haitakuwa rahisi kunigundua kutokana na mbinu zangu.

Nilikuwa mjanja sana na nilihisi kuwa ningeweza kuishi na waume wote wawili bila kujuana. Musa nilikuwa nimeshamzoea na nilijua ningeishi naye vipi. Wasiwasi wangu ulikuwa kwa Mustafa.

Kutoka siku ile ya ndoa yetu nikaanza rasmi kuishi kwa Mustafa. Nilikuwa nikimpigia simu mlinzi aliyekuwa akilinda nyumba yetu ya Kimara kumuulizia hali ya nyumbani.

Alikuwa akinieleza kuwa hali ilikuwa  shwari, hakukuwa na tatizo. Mara kadhaa nilimtumia pesa kidogo kwenye simu yake ili kujenga urafiki naye ingawa alikuwa hafahamu nilikuwa wapi.

Pale nyumbani nilikuwa nikizima simu yangu kila nilipokuwa na Mustafa. Mustafa akiondoka ndio huwasha simu. Baada ya kupita wiki moja nikataka niende nyumbani kwangu ili nifanye usafi.

Asubuhi moja nikamwambia Mustafa kuwa nitakwenda sokoni. Nilimwambia hivyo ili ajue kuwa sitakuwepo nyumbani kwa muda. Alipotoka tu na mimi nikatoka. Nilikodi teksi ikanipeleka nyumbani kwangu Kimara,

Nilifungua mlango nikaingia ndani. Nyumba ilikuwa inanuka joto. Nikaanza kufanya usafi na kuweka vizuri kila kitu. Niliporidhika nikatoka. Nilikwenda sokoni nikanunua nilivyonunua kisha nikakodi tena teksi iliyonipeleka Mbezi nyumbani kwa Mustafa.

Ulikuwa umepita mwezi mmoja Musa aliponipigia simu. Alinipigia simu usiku. Siku hiyo nilisahau kuzima simu. Nilikuwa jikoni ninapika. Kwa bahati njema Mustafa alikuwa anaoga.

Nikaipokea ile simu haraka.

“Hello!” Nilisema kwenye simu kwa sauti ya hofu.

“Hello Mishi, habari ya huko?’ Musa akaniuliza.

“Nzuri, simu yangu inaisha chaji, tuzungumze haraka haraka. Ndio unakuja.”

“Niko mpakani, nitaondoka kesho alfajiri.”

“Utafika hapa saa ngapi?’

“Sijajua safari itakavyokuwa, ninaweza kufika usiku.”

“Sawa.”

“Salama lakini?”

“Salama tu.”

“Unafanya nini?”

“Ninapika.”

“Sawa. Ni hapo kesho.”

“Nakutakia safari njema.”

Musa akakata simu.

Sikutaka kuizima tena ile simu kwa vile nilijua Musa asingepiga tena, nikaiacha.

Wakati natoa chakula mezani, Amina naye akanipigia.

Nikapoke simu yake.

“Leo kama bahati kukupata,” akaniambia.

“Kwanini?” Nikamuuliza kwa wasiwasi.

“Kila nikikupigia hupatikani na nikija nyumbani hupo.”

“Ulikuja nyumbani lini shoga?”

“Ninakuja mara kwa mra lakini  ninakuta hupo na nikipiga simu hupatikani.”

“Simu yangu iliharibika. Leo ndio nimekwenda kuichukua kwa fundi,” nikamdanganya.

“Si ununue nyingine tu.”

“Pesa iko wapi shoga!”

“Kwani mume wako hakupi?”

Amina aliposema hivyo nikageuza uso wangu kutazama kwenye mlango wa chumba chetu. Niliogopa kwamba Mustafa anaweza kutokea ghafla na kutusikia.

“Amina nitakupigia baadaye tuzungumze, niko jikoni na tui linafufurika…” Nikabadili mada ghafla.

“Utanipigia saa ngapi?”

“Saa tatu utakuwa umelala?”

“Hapana. Nitakuwa bado nipo macho.”

“Basi nitakupigia, usijali.”

“Poa.” Amina akaniambia na kukata simu.

Nikaizima simu na kuiweka juu ya meza. Nilipomaliza kutoa chakula nilikwenda kumuita Mustafa chumbani.

“Chakula tayari,” nikamwambia.

“Sawa, nakuja.”

“Kwani unafanya nini?”

“Nimekwambia nakuja.”

Nikatoka mle chumbani. Wakati nakaa kwenye kiti Mustafa naye akatoka na kuja kukaa kwenye kiti.

Nilitenga chakula kwenye sahani nikamnawisha mikono kisha tukaanza kula.

Wakati tunakula tulikuwa tunazungumza hiki na kile. Tulipomaliza Mustafa aliinuka na kwenda kuketi seuleni. Mimi niliondoa vyombo na kuvipeleka jikoni kisha nikamfuata Mustafa sebuleni.

Alikuwa akiangalia tv lakini nilipofika nilizima tv nikawasha deki na kuweka CD ya filamu ya Kihindi. Nilikuwa mpenzi sana wa filamu za Kihindi.

Mustafa alipoona naweka CD akaniuliza.

“Unaweka nini tena?”

“Naweka filamu ya Kihindi.”

“Mimi nilikuwa nataka kutazama taarifa ya habari.”

“Achana na taarifa ya habari, ngoja tuangalie filamu, ni nzuri. Wewe mwenyewe utaipenda.”

“Tatizo si kuwa ni nzuri au mbaya, mimi sina ushabiki wa filamu za Kihindi. Sasa utakuwa unaangalia wewe peke yako.”

“Acha wewe…tutaangalia sote.”

“Nakwmbia kweli Mishi. Mimi siangalii filamu za Kihindi.”

“Basi anza leo kungalia, utaipenda.’

Hayo ndio maisha yetu yalivyokuwa, matani, mizaha na ukweli vilikuwa vitu vya kawaida kwetu.

Usiku ule sikuwasha tena simu na hivyo sikumpigia tena Amina kama nilivyomuahidi.

Wakati nimelala na Mustafa nilikuwa nikimuwaza Musa. Nilikuwa nikijiambia nitawezaje kuondoka pale nyumbani kesho yake na kurudi nyumbani kwangu pindi Musa atakapokuwa amerudi

Nikajiuliza nitamuaga Mustafa ninakwenda wapi ambapo nitakaa hadi Musa atakapoondoka tena. Kwa jinsi nilivyomchunguza Mustafa tangu tulipooana hakutaka kuwa mbali na mimi na wivu ulikuwa mwingi sana.

Inaendelea...

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST