HADITHI: Bomu Mkononi - 16

3 months ago 40

UFUNDI wote niliofundwa kwa kungwi nilipanga kuumalizia kwake ili nihakikishe kuwa Mustafa anakuwa haoni wala hasikii juu yangu. Na itakapokuwa hivyo nitajihakikishia kuwa gari ninalipata tu, Mustafa hatakuwa na ujanja!

Asubuhi kulipokucha baada ya kumaliza kazi zangu za nyumbani nilimpigia simu Musa kujua kama angekuja siku ile.

Nilipomuuliza kama anakuja akanijibu kuwa hakuwa na uhakika wa safari

“Kwanini?” Nikamuuliza.

“Tajiri hataki gari lirudi tupu na mpaka sasa sijapata mzigo.”

“Kwa hiyo kuna uwezekano usirudi leo?” Nikamuuliza.

“Uwezekano huo upo.”

“Basi utanijulisha itakavyokuwa.”

“Sawa.”

Baada ya kukata simu nikampigia shoga yangu Amina.

“Amina vipi?” Nikamuuliza Amina baada ya kupokea simu yangu

“Poa Mishi, za kunisusa?”

“Sijakususa shoga, naona wewe ndio uko kimya.”

“Kawaida tu shoga, si unajua mishemishe?”

“Mishemishe zipi hizo shoga yangu? Tuambiane.”

“Hizo hizo za kuganga njaa, kwacha hakuchi.”

“Mbona kwacha shoga na njaa imeshakuwa shibe,” nilimwambia hivyo kimzaha kisha nikacheka na yeye akacheka.

“Hiyo shibe iko wapi?” Akaniuiza baada ya kicheko

“Usinidanganye, kwani shem wangu hayupo?”

“Nani Shabir?”

“Huyo huyo au una mwingine?”

“Mwingine wa nini shoga, mimi ndio nimeshafika pale na yeye ameshafika hapa!”

“Wacha!”

Tukacheka.

“Kwa hiyo bado mnaendelea?”

“Tupo pamoja. Alikuwa amekwenda Arusha ameniambia atarudi mchana huu.”

“Akirudi mtakuwa wapi?”

“Ataniambia yeye.”

“Lini atakwenda nje?”

Niliskia akisema atakwenda wiki ijayo.”

“Ataondoka na Mustafa?”

“Mh! Naona wale wana hatari ya kutengana, kila mmoja atabaki kivyake.”

Nikashituka

“Kwanini?”

“Shabir analalamika kwamba anapomuachia kazi Mustafa haoni faida.”

“Shabir analalamika kwamba anapomuachia kazi Mustafa haoni faida.”

“Yaani Mustafa anamtia hasara?”

“Ndiyo maana yake.”

“Kwa maneno mengine ni kwamba anamuibia, si ndio?”

“Mh! Siwezi kujua kazi zao zinavyokwenda.”

“Na ndio kama hivyo ulivyosema kuwa wanaweza kutengana?”

“Uwezekano huo upo kwa sababu Shabir analalamika sana.”

Nikashusha pumzi. Kimoyomoyo nilijiambia ukweli nitaupata kwa Mustafa mwenyewe.

Baada ya kuzungumza kwa kirefu na Amina tuliagana nikakata simu.

Nikabaki na mawazo. Kama Shabir na Mustafa wanataka kufarikiana, kila mmoja afanye kazi kivyake, Mustafa atamudu kweli kuwa peke yake wakati anategemea nguvu za Shabir? Nikajiuliza.

Nikaendelea kujiambia kama watafarikiana huenda ukawa ndio mwisho wetu kwani nisingeweza kuendelea kuwa naye kama atakuwa hana pesa.

Lakini ukweli wote nitaupata kwa Mustafa mwenyewe, nikajiambia. Amina sikumuamini sana. Anaweza kuwa ananidanganya.

Dukuduku la kutaka kujua ukweli likawa limenipata. Nikajikuta nampigia simu Mustafa ingawa sikikuwa nimepangia kumpigia muda ule

“Habari yako baby?” Nikamsalimia Mustafa kwa pupa mara tu alipopokea simu yangu

“Safi, vipi Mishi?” Mustafa akaniuliza. Ingawa sauti yake ilikuwa imechangamka haikuwa ya kawaida. Ilionyesha alikuwa na kitu.

“Mie niko poa, sijui wewe.”

“Mimi vilevile niko poa, niambie…”

“Uko wapi?” Nikamuuliza baada ya kukosa la kusema.

“Niko nyumbani. Nilikuwa nafanya usafi kidogo.”

“Shabir hajambo?” Nikamchokoza kusudi.

“Hajambo,” akanijibu.

“Au hamjakutana?” Nikaendelea kumchokoa

“Sijakutana naye tangu juzi, alienda Arusha kumtazama mama yake.”

“Kumbe yuko Arusha?” Nikajifanya sijui.

“Lakini anaweza kurudi leo.”

Nikatamani kumuuliza kama walikuwa na mgogoro lakini sikujua ningeanzia wapi. Nikabaki kujiuma uma midomo.

“Nilikuwa na shida,” nikamwambia baada ya kuamua kubadili ile mada.

“Shida gani?”

“Nilikuwa na shida ya shilingi laki moja.”

“Nitakupatia lakini subiri nikienda benki.”

“Utaenda muda gani?”

“Nikitoka nyumbani nitaenda benki.”

“Basi unirushie kwenye simu yangu.”

“Sawa.”

Nikamuaga kisha nikakata simu.

Ilikuwa imefika saa nane nilipoona meseji ya Mustafa ya shilingi laki moja alizonitumia kupitia simu yangu. Nikaamua kuziacha humo humo.

Ilipofika saa kumi nikaenda kumtembelea shangazi yangu Magomeni.

Kama ambavyo nilimsingizia ugonjwa kwa mume wangu, kweli nikamkuta anaumwa.

Alikuwa amelala chumbani mwake akiugulia kitandani.

“Unaumwa na nini shangazi?” Nikamuuliza.

“Presha imekuja juu tangu asubuhi, sijisikii vizuri.”

“Mbona hukuniarifu shangazi, si una simu yako?”

“Ilianza kidogo kidogo tu lakini huu mchana ndio nikawa hoi.”

“Umekwenda hospitalini?”

“Sijakwenda ila nimemeza dawa tu. Nilikuwa na tembe zangu za kutuliza presha.”

“Sasa unajisikiaje?”

“Sijambo kidogo.”

“Mara nyingine ukijisikia kuumwa nipigie simu nije, usinyamaze.”

Shangazi akanyamaza kimya. Baadaye akaniuliza.

“Mumeo hajambo?”

“Hajambo.”

“Hajakwenda safari?”

“Yuko Mwanza. Alikwenda jana.”

“Atarudi lini?”

“Labda kesho.”

Shangazi aliendelea kuniuliza jinsi tulivyokuwa tunaishi na mume wangu, nikamwambia kuwa tulikuwa tunaishi vizuri. Nilikaa kwake hadi saa moja usiku. Nilikuwa nimempikia chakula na kumtengea ndipo nilipomuaga na kuondoka.

Saa nne usiku nikiwa nyumbani kwangu ndipo Musa alinipigia simu akaniuliza hali yangu na hali ya shangazi, nikamwambia shangazi amepata nafuu lakini ana tatizo jingine la presha.

“Nilikuwa kwake tangu jioni lakini kwa sasa ana nafuu kidogo,” nikamwambia.

Musa akaniambia kwamba walikuwa wameshapata mzigo ambao wataupakia kesho yake na kwamba wangeondoka alfajiri ya keshokutwa kurudi Dar, nikamjibu. “Sawa”

Siku iliyofuata nilimpigia simu shangazi kujua hali yake akanijibu kuwa ameamka vizuri.

“Sasa nisije?” Nikamuuliza

“Hapana, leo sitaki msaada, najiskia vizuri.”

“Sawa shangazi.”

Siku ile nilishinda nyumbani tu, sikwenda popote. Alfajiri ya siku iliyofuata Musa akanipigia simu kunijulisha kuwa wanaondoka Mwanza kurudi Dar.

Musa alipofika Dar nikakata mawasiliano yangu na Mustafa. Wakati wote Musa alipokuwa nyumbani nilikuwa nikimuombea apate safari aondoke. Siku ya nne yake dua yangu ikakubaliwa, Musa akapata safari ya Burundi.

Alipoondoka tu mishemishe zangu na Mustafa zikaanza. Sasa tulikuwa hatukutani tena kwenye mahoteli, nilikuwa nikienda nyumbani kwake asubuhi na kurudi nyumbani kwangu jioni.

Ulikuwa ni unyumba wa kupika na kupakua. Nilikuwa napika chakula nyumbani kwake, tunakula na wakati mwingine tunatoka na gari kwenda kutembea.

Kitendo ambacho nilijitahidi kukikwepa ni kulala kwa Mustafa kwa sababu niliogopa endapo nitalala nje, nyumbani kwangu kutakuwa hakuna mtu na wezi wanaweza kuja kuvunja nyumba usiku.

Siku moja nikamuuliza Mustafa kuhusu safari zake za nje, akaniambia kulikuwa na mabadiliko kidogo, badala ya kwenda yeye anakwenda mwenzake Shabir.

“Kwanini?” Nikamuuliza.

Hapo hakunipa jibu isipokuwa aliniambia wanapeana zamu. Nikahisi kulikuwa na kitu.

Siku nyingine akaniambia anaanzisha safari zake mwenyewe lakini kwanza alitaka akanitolee posa nyumbani kwatu ili tuoane.

“Nimeona unafaa kuwa mke wangu,” akaniambia. Kauli yake ambayo sikuitarajia ilinishitua.

“Unataka tuoane?” Nikamuuliza.

“Una sifa za kuwa mke wangu.”

“Mh!”

“Mbona unaguna?”

“Umenifanyia surprise!”

“Hapana. Nadhani ulikuwa unafahamu wakati wote tulikuwa katika maandalizi ya uchumba.” Mustafa akaniambia.

“Mbona hukuwahi kuniambia.”

“Kule kukubaliana kwetu kuwa tunaishi pamoja inatosha kuwa ni taarifa kwetu sote kuwa wakati wowote tunaweza kuoana. Ulitaka nikuambie nini zaidi ya hapo?”

Nikawa sina la kusema. Kwa kweli nilishindwa kumwambia kuwa nilikuwa na mume wangu, asingenielewa na pia malengo yangu ya kuendelea kuwa naye yasingekuwepo tena.

“Niambie baby, sifai kuwa mume wako mtarajiwa?” Akaniuliza baada ya ukimya mfupi.

Nikainua uso wangu niliokuwa nimeuinamisha, nikamtazama kisha nikamjibu.

“Unafaa.”

“Au una mwingine zaidi yangu?”

Nikatikisa kichwa haraka.

“Sina mwingine zaidi yako.” Nilipomwambia hivyo sauti yangu mwenyewe ilinisuta kwa kusema uongo. Ilitoka ikiwa haina nguvu. Kama angekuwa na akili nzuri angegundua kama namdanganya.

Itaendelea...

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST