HADITHI: Bomu Mkononi - 15

3 months ago 37

By  Faki Faki

Mwananchi Communications Limited

MUSTAFA akanipa shilingi laki mbili. Baada ya kuniacha hapo nikarudi nyumbani. Nilikuwa nimechoka lakini nilikuwa na furaha kwamba kesho yake nitafanyiwa shopping.

Simu yangu nilikuwa nimeizima muda wote niliokuwa kwa Mustafa ili Musa asije akanipigia, siri ikatoka. Kwani Mustafa angejua kuwa nina mume na mimi sikutaka ajue.

Nilipofika nyumbani ndipo nilipowasha simu. Nikawa na wasiwasi kwamba huenda Musa alikuwa akinitafuta kwenye simu mchana kutwa.

Nikapanga uongo kwamba endapo atapiga na kuniuliza kwanini nilikuwa sipatikani nimdanganye kuwa simu niliiacha kwenye chaji na mimi mwenyewe nilikuwa nimekwenda kwa shangazi ni mgonjwa.

Lakini Musa hakupiga simu hadi saa tatu usiku.

“Hello…vipi?” Akaniuliza.

“Poa. Mko wapi?” Nilikimbilia kumuuliza hivyo kwa kuzuga tu. Sikuwa na shida ya kujua yuko wapi.

“Tuko njiani lakini tunakaribia kufika.”

Nilikuwa nasubiri aniambie kuwa simu yangu ilikuwa haipatikani ili nimpe uongo wangu lakini hakuniambia.

“Hukuwahi kunipigia mchana?” Kiherehere changu kikanifanya nimuulize.

“Sikuwahi kukupigia. Sasa hivi tunakula chakula ndio nimekupigia.”

“Mnakula nini?”

“Ugali na kuku.”

“Poa. Sasa mtaondoka saa ngapi hapo?”

“Muda wowote tu tutakaoamua.”

“Sawa. Nawatakia safari njema.”

“Poa.”

Musa akakata simu.

Siku iliyofuata niliamka na mawazo ya kwenda shopping. Nilishawahi kwenda shopping mara kadhaa nikiwa na Musa lakini sikujua ni kwanini kupelekwa shopping na mwanaume wa nje kulinifurahisha.

Ilipofika saa nne tu nikampigia simu Mustafa.

“Vipi?” Nikamuuliza alipopokea simu yangu.

“Poa. Ndio unataka kutoka?” Akaniuliza.

“Ndio. Ni kuhusu ile safari yetu.”

“Basi subiri kidogo nitakupigia.”

“Poa.”

Nikakasirika. “Mustafa naye anapenda kupoteza muda!” Nikalalamika peke yangu.

Nilisubiri hadi saa sita Mustafa akanipigia simu.

“Nikufuate wapi?” Akaniuliza.

“Pale uliponiacha jana.”

“Nakuja.”

Nilikuwa nimeshajitayarisha kwa kutoka. Nilikwenda kujitazama kwenye kioo kujiridhisha kisha nikatoka. Nilifunga mlango wangu nikaenda katika ule mtaa alioniacha Mustafa jana yake.

Hapo napo nilisubiri sana. Mpaka Mustafa anatokea na gari lake ilikuwa karibu saa saba. Nilikuwa nimechukia lakini nilipoliona gari hilo nikatabasamu.

Mustafa aliposimamisha gari nikafungua mlango wa upande wa pili wa dereva na kujipakia.

“Mbona umechelewa sana?” Nikamuuliza.

“Nilikuwa na Shabir. Si unamjua Shabir mazungumzo yake hayaishi. Anazungumza na kuyarudia hayo hayo.”

“Kwanza twende tukale hotelini, sikupika kwa ajili ya kukusubiri wewe.”

“Usijali.”

Tukaenda katika hoteli moja iliyokuwa pale pale Kimara. Baada ya kula chakula tukatoka tena.

Tulikwenda katika maduka ya barabara ya Samora.

“Utahitaji nini?” Mustafa aliniuliza wakati tukiingia katika duka moja.

“Vitu vingi tu.” Sikuona aibu kumwambia hivyo. Nilikuwa nimeshamzoea.

“Kama nini na nini?”

“Nguo, viatu, vipodozi…”

“Punguza kidogo. Nimechukua laki saba tu.”

“Itatosha.”

“Ninataka ibaki.”

“Itabaki.”

Tulipoingia katika duka hilo ambalo lilikuwa la mavazi ya wanawake na vipodozi nilinuua jozi moja ya viatu, magauni matatu, mawigi mawili na vipodozi mbalimbali.

Sikujua Mustafa alilipa kiasi gani. Tukarudi kwenye gari. Nilikuwa nataka nirudi nyumbani lakini Mustafa akanipeleka nyumbani kwake.

“Mbona tumekuja huku?” Nikamuuliza.

“Kumbe ulitaka twende wapi?” Mustafa akaniuliza.

Nilishindwa kumjibu kuwa nilitaka anirudishe nyumbani. Nikabaki kujiuma uma midomo.

“Ulikuwa na shughuli ya kufanya?” Mustafa akaniuliza tena.

“Ninayo.” Nikamjibu kwa sauti iliyonywea huku nimeinamisha uso wangu

“Shughuli gani?”

Sikuwa na jibu kwa vile sikuwa na shughuli yoyote. Badala yake nikamuuliza.

“Kwani tutakaa hapa hadi saa ngapi?”

“Unauliza saa ya nini?” Mustafa aliniuliza huku akishuka kwenye gari. Na mimi nikashuka.

Tukaingia ndani.

“Nimeshakuwa na wasichana wengi lakini napatwa na mvuto wa ajabu ninapokuwa na wewe. Sijui ni kwanini?” Mustafa akaniambia wakati tumeketi sebuleni.

“Ni kwa sababu ya mapenzi.” Nikamwambia.

“Umegundua kuwa ninakupenda sana?”

Nikabetua mabega yangu.

“Sijagundua hilo, hujanionesha bado kuwa unanipenda sana.”

“Ulitaka nikubebe ndio ugundue kuwa nakupenda sana.” Mustafa akaniambia huku akiinuka na kunifuata.

“Sasa ngoja nikubebe.”

Mustafa akainama na kunichota.

“Hebu bwana! Mustafa mbona uko hivyo…wewe akili zako zikoje?” Nikapiga kelele.

Wakati huo alikuwa ameshanichota na kunibeba mzima mzima.

Nikabaki kucheka.

“Nataka ugundue kuwa nakupenda sana,” akaniambia.

“Ninunulie gari ndio nitajua unanipenda sana.”

Mustafa alinisogeza karibu na midomo yake akanipiga kisi cha midomoni huku nikiwa mikononi mwake.

“Nitakununulia, subiri nikienda Japan.”

“Utakwenda lini?”

“Nitakwambia. Bado kwanza.”

Mustafa baada ya kunibeba aliniingiza chumbani kwake akanitupa kwenye kitanda. Kumbe alikuwa na lake.

Maji ukiyavulia nguo yaoge. Niliyataka mwenyewe ilibidi nikubaliane nayo, nikakubaliana nayo.

*******

Usiku ulinifikia nikiwa nyumbani kwa Mustafa. Tuliondoka saa mbili usiku. Tukaenda katika hoteli iliyokuwa jirani kula chakula kisha akanirudisha Kimara.

Nilipofika nyumbani ilikuwa karibu saa tatu na nusu. Niliingia chumbani mwangu. Nikauweka kitandani mkoba wangu pamoja na mfuko uliokuwa na vitu nilivyonunuliwa.

Nilivua nguo nilizokuwa nimevaa nikaanza kuvaa zile nilizotoka dukani. Nilizijaribu zote pamoja na viatu huku nikajitazama kwenye kioo. Nguo hizo pamoja na vile viatu vilinipendeza sana.

Niliporidhika, nilivua nguo hizo nikaziweka kabatini. Ndipo nilipokumbuka kwamba nilikuwa nimezima simu kutoka mchana. Nikaitoa kwenye mkoba na kuiwasha.

Muda ule naiwasha Musa akanipigia.

Nikaipokea.

“Hello Baby!” Nikajidai kumwambia kwenye simu.

“Mbona ulikuwa hupatikani?” Musa akaniuliza.

“Ulinipigia saa ngapi?”

“Nimekupigia mara nyingi tu kutoka mchana.”

“Ni kweli. Nilikwenda kwa shangazi, niliarifiwa kuwa alikuwa anaumwa. Simu nikaiacha kwenye chaji.”

“Mbona hukuniambia?”

“Simu iliisha chaji na nilidhani ningewahi kurudi ili nikufahamishe lakini ndio nimerudi sasa.”

“Anaumwa sana?”

“Nilivyoondoka alikuwa amepata nafuu, lakini nilipokwenda alikuwa na hali mbaya. Nilimpeleka hospitalini akawekewa dripu, ndio maana nimechelewa.”

“Ana nini, malaria?”

“Ndio, ana malaria.”

Wakati nasema uongo huo nilikuwa nimejishika mdomo kama vile nilikuwa naogopa kuwa angegundua kuwa namdanganya.

“Mpe pole, nikirudi nitakwenda kumuangalia.” Musa akaniambia baada ya kuukubali uongo wangu.

“Lakini kwa sasa hajambo?”

“Kesho utakwenda tena.”

“Itabidi niende nikamjulie hali.”

“Basi utanijulisha anavyoendelea.”

“Poa. Uko wapi?”

“Niko Mwanza.”

“Mmefika salama?”

“Tumefika salama.”

“Mnatarajia kurudi lini?”

“Labda kesho.”

“Sawa. Basi usiku mwema.”

“Na kwako pia.”

Musa akakata simu.

Licha ya kufanikiwa kumdanganya Musa, nilipata wasiwasi kuwa endapo atarudi na kunitaka twende kwa shangazi halafu akakuta shangazi hakuwa akiumwa itakuwaje?

Nikajiambia ataona kwamba nilimdanganya. Na atatafuta sababu kwanini nilimdanganya. Atagundua kuwa nilikuwa nimekwenda sehemu!

Nilipowaza hivyo nilianza kupata hofu.

Hofu yangu haikunizuia nisimuwaze Mustafa ambaye nilikuwa nimempenda zaidi ya Musa. Nataka niwe sahihi kwamba mapenzi yangu kwa Mustafa yalikuwa na sababu za kiulimbukeni. Ulimbukeni wa pesa na maisha ya kifahari.

Nilikuwa nikifikiria kwamba kama nitaendelea kuwa na Mustafa nitaweza kujenga nyumba yangu mwenyewe na pia kununua au kununuliwa gari.

Pia nilifikiria kwamba nikiwa na Mustafa pesa haitanipiga chenga kwa sababu Mustafa kwa jinsi nilivyomfahamu hakuwa tajiri lakini alikuwa mtafutaji na niliamini msemo wa Kiswahili kuwa mkaa karibu na waridi haachi kunukia.

Usiku wa siku ile niliwaza kununuliwa gari na Mustafa kama alivyoniambia. Sikujua kama maneno yake yalikuwa ya utani au ya ukweli lakini mimi niliyachukulia kuwa ni ya kweli. Hata kama yeye aliyasema kiutani mimi nitayafanya kuwa ya kweli kwani nilikuwa nimepanga kumtia mikononi vilivyo.

Inaendelea…

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST