HADITHI: Bomu Mkononi - 14

3 months ago 34

By  Faki Faki

Mwananchi Communications Limited

Nilipofungua mlango nilimpokea Musa begi lake kwa vile aliniahidi kuniletea zawadi, nikaingia nalo ndani.

“Habari za safari?” Nikamuuliza.

“Nzuri, za hapa?”

“Hapa ni kwema tu.”

Wakati tunaulizana hali na Musa nilikuwa nimeshalifungua begi na kuanza kutoa vilivyokuwemo ndani.

Nikaona boksi, nikalitoa na kulifungua. Lilikuwa na viatu vizuri vya kike vya mchuchumio.

Nikahisi kwamba ilikuwa ndio zawadi yangu. Kile kitendo cha kupekua begi lake hakikumshangaza Musa kwani kilikuwa cha kawaida. Kama kilimkera hakuweza kuniambia kwa sababu alikuwa akinipenda sana.

“Hii ndio zawadi yangu?” Nikamuuliza huku nikitabasamu baada ya kuona vile viatu.

“Ndiyo hiyo.” Musa akaniambia.

Hapo hapo nikaanza kuvijaribu miguuni. Vilikuwa sawa kabisa. Nikanyanyuka na kujaribu kuvitembelea pale sebuleni.

“Vimekupendeza sana.” Musa akaniambia.

“Sema kweli?”

“Nakwambia kweli kabisa.”

“Siku nyingine uniletee mkoba wa kike wa rangi hii hii ili niweze kumechisha.”

“Nitakuletea na gauni lake.”

“Utakuwa umefanya jambo la maana sana.”

Baada ya kuvijaribu vile viatu nilivivua nikamwambia mume wangu aende akaoge ili tule chakula.

Musa akaingia chumbani. Alipomaliza kuoga alikuja mezani tukala chakula kisha tukakaa sebuleni kuzungumza. Muda wa kulala ulipowadia tukaenda kulala.

Asubuhi iliyofuata, Musa baada ya kunywa chai alitoka kwenda kazini kwake. Nilipoona ameondoka ndipo nilipowasha simu.

Wakati nawasha meseji ikaingia. Ilikuwa meseji ya Mustafa ilisema.

“Mbona hupatikani?”

Nikaijibu haraka.

“Nilikuwa nachaji simu.”

Wakati naosha vyombo Mustafa akatuma meseji nyingine.

“Niko njiani naenda Arusha, nitarudi kesho.”

Na mimi nikamuuliza.

“Kuna nini?”

“Nakwenda kumjulia hali mama yake Shabir.” Hilo ndilo jibu alilotuma Mustafa. Nikamtumia meseji nyingine.

“Ukirudi utanishitua.”

Mustafa akanijibu. “Poa.”

Nilipomaliza kuosha vyombo nilikwenda kuoga kisha nikakaa sebuleni kuangalia televisheni.

Ni kweli kuwa mapenzi hayagawanyiki na mtu huwezi kupenda watu wawili kwa wakati mmoja. Mawazo yangu yote yalikuwa kwa Mustafa. Musa hakuwa na nafasi tena ndani ya moyo wangu. Tulikuwa pamoja tu kwa sababu alinioa lakini si kimapenzi.

Nilivyoanzana na Mustafa ilikuwa ni kwa sababu ya tamaa ya pesa baada ya kumuona shoga yangu Amina alikuwa akihongwa pesa nyingi na mwanaume wake. Lakini kwa sasa yalikuwa yamegeuka mapenzi. Nilikuwa nampenda sana Mustafa.

Nilikuwa natamani Musa asikae sana aondoke ili nipate nafasi ya kuwa na Mustafa. Moyo wangu tayari ulikuwa umeshaharibika. Nilikuwa namhadharisha Musa kuhusu wasichana huko anakosafiri, sasa tatizo lilikuwa kwangu mimi.

Kama nilivyokuwa nikitamani, Musa hakukaa sana. Baada ya siku tatu tu akaniambia anakwenda Mwanza. Nikafurahi kweli kweli kwani wakati ule Mustafa alishanijulisha kuwa alirudi kutoka Arusha na nilikuwa sipati nafasi ya kukutana naye.

Musa alipoondoka kwenda Mwanza nikampigia simu Mustafa.

“Uko wapi baby?” Nikamuuliza kwa kumlegezea sauti.

“Niko nyumbani,” akanijibu.

“Huko nyumbani kwako utanionyesha lini?”

“Siku yoyote tu utakayotaka.”

“Nataka unionyeshe leo.”

“Ni wewe tu.”

“Lakini nisije kupigwa na wanawake zako!”

“Hapana. Sina mwanamke yeyote humu ndani, ondoa wasiwasi.”

“Kwani unaishi wapi?”

“Niko Mbezi.”

“Sasa tutakutana wapi. Nimekumiss baby…?”

“Nikupitie nyumbani kwako?” Mustafa akaniuliza.

“Hapana. Hapa wambea wengi…”

“Hupendi nije kwako?”

“Napenda sana lakini sitaki umbea. Hapa pana umbea mwingi. Bora tukutane huko huko.”

“Kama wapi?”

“Nitakuja pale hotelii tulipokuwa juzi.”

“Nikufuate saa ngapi?”

“Nikifika hapo nitakupigia. Kwani kazi ya simu ni nini?”

“Ni kupigiana…”

“Basi nikifika nitakupigia.”

“Sawa baby.”

“Poa…”

Nikakata simu na kuanza kujitayarisha kutoka. Mle ndani nilikuwa naona kama niko jela. Baada ya nusu saa nilikuwa nimeshamaliza kuoga, kuvaa na kujitia manukato. Nikatoka kwenda saluni kutengenezwa nywele zangu.

Nikiwa hapo saluni Mustafa akanipigia simu.

“Uko wapi?” Akaniuliza.

“Niko saluni, nifuate hapa.”

“Iko sehemu gani?”

Nikamuelekeza mahali ilipokuwa saluni hiyo.

“Nakuja sasa hivi.” Mustafa akaniambia na kukata simu.

Haukupita muda mrefu sana, gari la Mustafa likasimama mbele ya saluni hiyo. Nililiona kupitia kwenye mlango ambao ulikuwa wa kioo. Nilikuwa nimeshatengezwa nywele zangu nikalipa pesa na kutoka.

Nilifungua mlango wa gari wa upande wa pili wa dereva nikajipakia.

“Vipi, kwema?” Mustafa akaniuliza huku akitia gia.

“Kwema,” nikamjibu.

Mustafa alikanyaga mafuta, gari likaondoka.

“Tunakwenda nyumbani.” Mustafa aliniambia wakati gari likiwa kwenye mwendo.

“Twende tu ila sitakaa sana.”

“Kwanini?”

“Ninataka nipaone tu nyumbani kwako na nipajue.”

“Kwa hiyo tuishie nje?”

“Ndani.”

“Kama ni ndani lazima ukae.”

“Mh!” Nikaishia kuguna tu, sikusema kitu tena.

“Kwanza twende hotelini tukale.” Mustafa aliniambia baada ya ukimya mfupi.

Tukaenda katika hoteli ile ile tuliyopanga kukutana.

Tulikula pilau ya kuku. Baada ya kula mwenzangu alianza kunywa bia. Alinilazimisha na mimi ninywe. Nilijaribu kuionja nikashindwa kuinywa baada ya kuona ilikuwa nzito na chungu.

Mustafa aliagiza Cocacola akanichanganyia bia na Cocacola ili niweze kunywa. Nilipojaribu tena nikaona afadhali kidogo nikaendelea kunywa lakini niliishia chupa moja tu. Nilijisikia kulewa na kichwa changu kilikuwa kizito.

Lakini badala ya kupumbaa nilichangamka na kuanza kuzungumza maneno yasiyo na kichwa wala miguu.

Mustafa alikuwa amekunywa chupa tatu za bia lakini alikuwa yuko sawa, akaniambia tuondoke. Tukaondoka.

“Sasa tunakwenda wapi?” Nikamuuliza.

“Tunakwenda nyumbani.”

Nikajidai naguna lakini heshima ya ile bia moja niliyokunywa nilikuwa ninaiona. Ilikuwa imenisisimua. Sikuwa na wazo jingine isipokuwa ni la kuvunja amri ya sita tu.

Tulipofika nyumbani kwa Mustafa niliiona nyumba yake. Ilikuwa nyumba nzuri iliyokuwa imezungushiwa ukuta uliojengwa kisasa ukipanbwa na taa za urembo na umezungushiwa uzio wa umeme (electric fence). Tulikuta mlinzi wa makampuni ya ulinzi aliyekuwa akivinjari kwenye geti.

Mustafa aliingiza gari ndani akaliegesha kwenye banda la gari. Tuliposhuka nilimuuliza.

“Hii ni nyumba yako mwenyewe?”

“Hapana, nimepangisha tu, yangu ninaijenga sasa Kigamboni.”

“Nilifikiri ni ya kwako mwenyewe.”

“Ya kwangu ikikamilika utakwenda kuiona.”

“Itakamilika lini.”

“Ujenzi bado unaendelea.”

“Sio mbaya siku ukinipeleka nikaone na ujenzi ulipofika.”

“Usijali, baby.”

Tulikuwa tumeshafika kwenye mlango, Mustafa aliufungua tukaingia ndani. Tulitokea katika sebule pana iliyokuwa na fanicha za thamani sana.

Nilikwenda kuketi kwenye sofa mojawapo nikajilaza kama vile nilikuwa mwenyeji wa nyumba ile.

“Mustafa hebu niambie unaishi na nani ndani ya nyumba hii?’ Nikamuuliza kwa ukali kidogo.

“Ninaishi peke yangu.” Mustafa akanijibu huku akija kuketi pale nilipokuwa nimejilaza.

“Nani anayekufanyia usafi?”

“Nafanya mwenyewe.”

“Unaposafiri hii nyumba unamuachia nani?’

“Namuachia mlinzi, si umemuona pale nje?”

“Sasa kwanini hutaki kuoa?’

“Bado bado kwanza.”

“Mpaka lini?”

“Tutazungumza baadaye.” Mustafa aliniambia huku akinyanyuka akanishika mkono na kuninyanyua.

“Twende chumbani, tuna mengi ya kuzungumza kuliko hayo.”

Mustafa akaniingiza chumbani kwake. Nilipoona kitanda tu nikajilaza hapo hapo.

Kilichofuatia baada ya hapo hakisemeki.

******

Niliondoka nyumbani kwa Mustafa saa moja usiku. Nilitaka kuondoka mapema lakini Mustafa alinizuia, akataka nilale hapo hapo. Nikamkatalia.

Kule kubishana kukatufikisha saa moja usiku. Alinipakia kwenye gari akanirudisha katika ule mtaa ulio jirani na mtaa ninaoishi. Katika mazungumzo yetu ya ndani ya gari aliniahidi kuwa angenifanyia shopping kesho yake.

“Tukutane saa ngapi?” Nilimuuliza.

“Nitakufahamisha kwenye simu muda wa kukutana,” akaniambia.

“Basi usisahau.”

“Nikisahau utanikumbusha.”

“Nitakupigia kwenye saa nne hivi.”

“Sawa.”

Inaendelea…

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST