HADITHI: Bomu Mkononi - 13

3 months ago 34

By  Faki Faki

Mwananchi Communications Limited

Sehemu ya 13

“HAWATAJUA, usijali.”

Tukiwa hapo hotelini nilishuhudia Mustafa akinywa chupa nne za pombe mbele ya macho yangu. Sikujua alizotangulia kunywa kabla yangu zilikuwa chupa ngapi. Licha ya kuonekana kuwa amelewa bado alikuwa yuko makini.

Baadaye aliinuka kwenye kiti na kuniambia.

“Njoo huku.”

Alinishika mkono. Nikainuka na kumfuata. Tulipanda ngazi hadi ghorofa ya kwanza. Kumbe Mustafa alikuwa amepangisha chumba maalum kwa ajili yangu. Chumba hicho kilikuwa katika ghorofa ya kwanza, tukaingia ndani.

Siku ile kwa mara ya kwanza tangu nilipoolewa na Musa niliisaliti ndoa yangu kwa kuvunja amri ya sita kwa sababu ya tamaa ya pesa na kutaka makuu.

Mustafa alinitoa usiku lakini nililamba shilingi laki tano. Alinifikisha na gari mahali pale pale aliponifikisha jana yake akanipa pesa hizo kisha akaondoka na gari lake.

Nilipofika nyumbani nilioga kisha nikaketi sebuleni kwangu na kumpigia simu Amina ili nijue kama anafahamu nilikuwa wapi.

“Amina vipi?”  Nikamuuliza alipopokea simu.

“Poa.” Amina alinijibu kwa sauti nzito iliyochoka.

“Uko wapi?” Nikamuuliza baada ya kusikia sauti yake iko vile.

“Niko hotelinini, nimelala,” akaniambia.

“Upo na mzee?”

“Haswaa…!”

“Amina umelewa wewe.”

“Kwanini?”

“Mbona unanijibu hivyo halafu sauti yako ni nzito.”

Amina akacheka.

“Mambo ya Reds hayo!” Akaniambia.

“Nilijua tu, kwa maana wewe siku hizi hushikiki.”

“Uko wapi Mishi?” Amina akaniuliza.

“Niko nyumbani, niende wapi shoga yangu.”

“Salimiana na shemeji yako.”

Hapo hapo nikaisikia sauti ya Shabir.

“Mishi vipi?”

Ilikuwa sauti iliyoonesha wazi kuwa Shabir alikuwa amelewa chakari.

“Naona upo na shoga yangu,” nikamwambia.

“Ndio tunakula raha tu…”

“Mkila raha msitusahau na sisi…”

“Njoo basi shemeji yangu unywe bia.”

“Mimi situmii kilevi.”

“Acha utoto wako… unataka unywe soda…?” Shabir akanichachamalia. Jinsi sauti yake ilivyokuwa kali nilihisi angenitukana.

Bila shaka Amina alimnyang’anya simu alipomuona anaanza kuropoka. Nikaisikia sauti ya Amina akisema.

“Jamaa yuko njwii hapa, hajui anachokisema, poa basi.”

Aliponiambia hivyo akakata simu japokuwa mimi ndiye niliyempigia.

Nikahisi kwamba Shabir alikuwa akimpa pesa nyingi Amina si kwa sababu alikuwa anazo, bali alikuwa analewa kupita kiasi. Hapo ndipo Amina anapompatia kwenye masuala ya pesa. Akimuomba kiasi chochote anampa.

Nikajiambia na mimi nikishazoeana na Mustafa nitamsubiri akilewa niwe ninamuomba pesa nyingi.

“Siwezi kuisaliti ndoa yangu bure bure, lazima kuwe na masilahi ya kutosha,” nikajiambia kimoyo moyo.

Wazo kwamba nini kitatokea endapo Musa atagundua kuwa nina mwannaume wa nje halikunjia akilini mwangu. Niliona kwamba ningeweza kuitunza siri ile na kwamba Musa asingeweza kuigundua kwa vile muda mwingi anakuwa safarini.

Sikujua ni kitu gani kilichonibadili ghafla, ni tamaa ya pesa au vile ninavyomkosa mume wangu kwa muda mrefu. Sikuweza kujua.

Sikukutana tena na Mustafa kwa siku tatu. Tulikuwa tukiwasiliana kwa smu tu. Asubuhi ya sku ya nne yake Amina akanipigia smu na kuniuliza kama mume wangu amerudi.

“Kwanini unaniuliza hivyo?” Nikamuuliza.

“Nataka nije nikutembelee.”

“Hajarudi, njoo tu.”

“Basi najitayarisha nije.”

“Nakusubiri.”

Baada ya kupita saa moja hivi Amna akafika nyumbani. Nilimkaribisha kwa furaha ili nipate umbea.

“Karibu shoga, nimekumiss…” Nilimwambia Amina alipoketi sebuleni.

“Hata mimi nimekumiss shoga. Tangu juzi nilikuwa bize na yule mwanaume. Jana ndio nimerudi nyumbani.”

“Acha shoga! Mlikuwa mwatumia tu…!”

“Yule jamaa anajua kuchezea pesa halafu sio mgumu.”

“Amekupa ngapi?”

“Kwanza zile zinazobaki baki tunaponunua vocha au anapolipia vyakula na ulevi, ninabaki nazo mimi. Mpaka naondoka jana nilikuwa na laki mbili halafu yeye mwenyewe amenipa milioni mbili. Juzi tukiwa pale pale hotelini alijisahau akanipa milioni moja. Jumla nimeondoka na milioni tatu na laki mbili. Nimeshaziweka benki.”

Alipotaja benki mwili ulinisisimka. Na mimi nilikuwa mbioni kufungua akaunti. Mustafa au Musa wakinipa pesa na mimi nilitaka niziweke benki kama mwenzangu.

“Naona tangu umpate bwana huyo mambo yako yanakuwa poa,” nikamwambia.

“Wala usiniambie shoga. Hivi namlilia aniletee pikipiki.”

“Kwanini asikuletee gari?”

“Gari bado kwanza, tumeanzana juzi juzi tu. Ataona nina tamaa.”

“Na vipi kuhusu Mustafa, hivi ana mke yule…?”

“Mbona unamuuliza, umempenda?”

Nikajidai kucheka.

“We Amina wanichekesha kweli…nimpende nini sasa wakati nina mume wangu?”

“Uliona wapi jiwe moja likainjika chungu?” Amina akaniambia.

“Hata mawili hayainjiki,” nikamjibu.

“Lakini yanakuwa afadhali kidogo.”

Nikabetua mabega yangu. Laiti Amina angekuwa na ujuzi tu wa kusoma akili ya mtu angegundua kuwa niliyabetua mabega yangu kumzuga tu.

“Mimi siko huko. Nimefundwa nikafundika. Nilikuwa nakuuliza tu.”

“Mustafa hajaoa bado.”

“Kama hajaoa atakuwa malaya sana,” nilimwambia hivyo kusudi ili anieleze tabia zake.

“Sijamjua bado, unajua hatuwi naye mara kwa mara.”

“Lakini nawaona wanapendana sana na Shabir.”

“Kawaida tu, unajua yule anatumwa na Shabir kwenda nje kumnunulia vitu na yeye anapata chake humo humo.”

Hayo ndiyo niliyokuwa nikiyataka.

“Hana shughuli nyingine?” Nikamuuliza.

“Ana maduka yake mawili pale Mwenge. Duka la spea za magari na duka la vipodozi.”

“Lakini yanamtosha.”

“Si umeona ana gari lake zuri.”

“Siku ile alinipakia hadi nyumbani.”

“Hakukutongoza?”

“Labda hakunipenda. Hakuniuliza chochote.”

“Alishindwa kwa sababu aliona tunafahamiana.”

“Labda.”

Siku ile Amina alishinda nyumbani kwangu, kwa hiyo tuliongea mengi kumuhusu Shabir na mwenzake Mustafa. Nilienda sokoni na Amina. Tuliporudi tulipika ugali na nyama tukala kisha tukaendelea na mazungumzo hadi jioni ambapo Amina aliniaga na kuondoka.

Licha ya kuzungumza mengi na Amina sikuthubutu kumueleza Amina kuwa jana yake niliisaliti ndoa yangu na Mustafa. Sikutaka Amina afahamu lolote na kama atafahamu iwe ni baadaye sana.

Usiri wangu huo kwa shoga yangu ulitokana na aibu. Ndoa yangu haikuwa na muda mrefu, hivyo niliona aibu kama Amina atajua kuwa natoka na Mustafa tena baada ya yeye kututambulisha siku ile pale hotelini.

Ilipofika usiku Musa akanipigia simu. Siku zote ninapopata simu ya Musa huwa nafurahi lakini siku ile kwa mara ya kwanza nilijisikia kuchukia.  Lakini sikujua ni kwanini.

“Hello Baby!” Musa aliita kwa bashasha baada ya kupokea simu yake.

“Niambie mume wangu?” Nikamwambia kwa kumzuga tu ili asijue kuwa mwenzake nimeshaota mbawa.

“Kesho nakuja mke wangu, niko mpakani.”

Kusema kweli sikutaka aje haraka. Hapo hapo nikanuna.

“Unakuja kesho?” Nikamuuliza nikijifanya sikumsikia vizuri.

“Kesho nakuja. Nimekumiss sana…”

Kwa jinsi moyo wangu ulivyonywea nilitaka ninyamaze tu lakini niliona nitamgutusha, nikajidai kumwambia.

 “Mimi zaidi…”

“Unaniambia ukweli mpenzi?”

“Kutoka ndani ya moyo wangu.”

“Wacha we…”

“Umeniletea zawadi gani?”

“Utakuja kuiona huko huko.”

“Nitafurahi.”

Nilikuwa kama ninayeigiza sinema. Maneno yangu hayakuwa na ukweli wowote. Sikuwa nimemmiss na wala sikuwa nikihitaji zawadi yake, kwa vyovyote vile zawadi yenyewe itakuwa nguo moja au vipodozi ambavyo hata mimi mwenyewe naweza kuvinunua.

Baada ya kuzungumza machache, Musa akaniaga. Nilichofurahi sio kwamba Musa anakuja bali kujua kama anakuja kwani angekuja ghafla bila kunifahamisha angeweza kukuta sipo nyumbani na hivyo kuanza kunitilia shaka.

Kesho yake Musa akanipigia simu saa kumi na mbili jioni akanijulisha kuwa ameshafika Dar na yuko ofisini kwao. Nikaandaa chakula kwa ajili yake. Saa mbili usiku Musa akawasili nyumbani.

Wakati Musa anabisha mlango nilizima simu yangu. Nilihofia kwamba Mustafa anaweza kunipigia simu wakati Musa akiwepo.

Inaendelea...

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST