HADITHI: Bomu Mkononi - 12

3 months ago 33

By  Faki Faki

Mwananchi Communications Limited

KABLA sijajibu, Mustafa akaongeza.

“Pesa si tatizo kwangu. Juzi juzi tu nilikuwa India. Nimekuja na pikipiki mia mbili.”

“Shabir alituambia wakati ulipompigia simu.”

“Huwa ninashirikiana naye.”

Wakati Mustafa akiniambia hivyo mawazo yangu yalikuwa mbali. Nilikuwa kwenye mjadala mkali ndani ya moyo wangu. Upande mmoja wa akili yangu ulitaka nimkubalie kwa sababu ya tamaa ya kupata pesa. Nilijua nikiwa naye pesa ya kuweka akiba haitanisumbua, nitakuwa kama Amina.

Lakini upande mwingine wa akili yangu ulisita kumkubalia kwa sababu nilikuwa mke wa mtu, kuwa na mwanaume mwingine wa pembeni ni jambo ambalo sikulizoea.

Jambo la ajabu ni kuwa wakati nikijadiliana na akili yangu kuhusu suala hilo nilikuwa nikipata ujasiri wa ajabu wa kumkubalia.

“We mkubalie tu... unaogopa nini… kwanza mume wako yuko safarini… akija akikaa siku tatu anaondoka tena, akienda huko anakaa mwezi mzima… Mustafa ana gari nzuri anakwenda nchi za nje mara kwa mara… huyo ndiye mwanaume wa kuwa naye…” Niliisikia sauti ikinishawishi ndani ya moyo wangu.

Nilijaribu kuipuuza kwa hofu ya kuisaliti ndoa yangu lakini sikuweza. Nikajikuta nikimuuliza Mustafa.

“Kwani wewe huna mke?”

“Mke wangu unaweza kuja kuwa ni wewe,” akaniambia na kunizidisha tamaa.

“Yaani huna mke?” Nikamuuliza tena ili nipate uhakika.

“Sijaoa bado.”

“Kwanini?”

“Kwa sababu sijampata anayenifaa.”

“Lakini mimi nisingependa kuolewa kwa sasa.”

Nilipotoa jibu hilo nilikuwa nimeshalegea. Nilikuwa kama ngamia niliyesalimu amri nikisubiri kuchinjwa tu.”

“Hata mimi sina nia ya kuoa kwa sasa. Nahitaji tu nipate mwenzangu wa kuniliwaza.”

“Bsi usijali, mimi nipo.”

“Utanionyesha mtaa unaoishi.”

“Nishushe tu hapa hapa.”

Sikutaka Mustafa anifikishe nyumbani kwangu na pia sikutaka aijue nyumba ninayoishi. Akasimamisha gari.

“Umeshafika nyumbani kwenu?” Akaniuliza.

“Tumekaribia lakini nataka nishuke hapa, kuna rafiki yangu nataka nimuone.’

“Sasa tutakutana lini tena?” Mustafa akaniuliza.

“Niambie wewe.”

Mustafa alifikiri kidogo kisha akaniambia.

“Nipe namba yako ya simu.”

Nikampa namba yangu na yeye akanipa yake.

“Kabla ya kunipigia kwanza nitumie sms,” nikamwambia.

“Usijali.”

Mustafa akanionyesha kuwa alikuwa amekusudia hasa kuwa na mimi, alitia mkono mfukoni akatoa pochi yake na kunipa shilingi laki moja.

“Asante,” nilimwambia huku nikizipokea pesa hizo.

“Basi wewe nenda, tutakuwa tunawasiliana.” Mustafa aliniambia.

Ajabu ni kwamba ile shilingi laki moja aliyonipa ilinifanya nianze kumpenda pale pale. Lakini wasiwasi wangu mkubwa ulikuwa kwa Amina. Nilikuwa na wasiwasi kwamba Amina anaweza kuja kumueleza Mustafa kuwa nina mume na kuniharibia mpango wangu. Kitu kingine pia sikutaka Amina afahamu mapema uhusiano wangu na Mustafa.

“Kuna kitu nataka nikwambie,” nikamwambia Mustafa.

“Kitu gani?” Akaniuliza.

“Nisingependa umueleze chochote Amina kwa sasa.”

“Kuhusu nini?”

“Kwani tumezungumza nini mimi na wewe?”

“Sawa. Nimekuelewa.”

Nikafungua mlango wa gari kisha nikamtupia jicho la tabasamu.

“Nakutarajia,” nikamwambia kabla ya kushuka.

Nikamuona Mustafa naye akitabasamu kisha akaliondoa gari. Nilisimama nikalitazama gari lake kwa nyuma lakini mawazo yangu hayakuwa kwenye gari, yalikuwa kwa mwenye gari.

Nilikuwa kama nimejisahau. Nilipozinduka nikaongoza njia kuelekea katika mtaa niliokuwa nikiishi.

Usiku ule mawazo yangu kwa mara ya kwanza yaliondoka kwa mume wangu yakawa kwa mwanaume mwingine ambaye nilimuona na kumfahamu kwa siku ile ile.

Sikutaka hata kupata muda wa kumdfahamu vizuri, madhali niliamini kuwa alikuwa ni mtu wa pesa, niliona kuwa atanifaa.

Nikiwa nyumbani kwangu nilikwenda kuoga, nilipotoka bafuni nikakaanga chipi zangu na mayai. Baada ya kula nilipumzika kidogo kisha nikaingia chumbani kwa ajili ya kulala.

Wakati nikiwa kitandani nililisajili jina la Mustafa kwa herufi moja tu ya M kwenye simu yangu. Hapo hapo nikamuona kwenye mtandao wa Whatsapp uliokuwa kwenye simu yangu.

Niliona picha yake akiwa amependeza. Na mimi nikatafuta picha nzuri kwenye sehemu ya picha nikaiweka kwenye WhatsApp yangu kisha nikamtumia meseji.

“Nimekuona,” nilimuandikia.

Haikupita hata dakika moja akatuma jibu.

“Na mimi nimekuona.”

Nikamtumia tena.

“Umependeza.’

Akanijibu. “Asante. Wewe pia umependeza.”

Tukaendelea kutumiana sms mpaka usingizi ulipoanza kuninyememelea tukaagana. Nililala huku moyo wangu ukiwa na furaha.

Siku ya pili yake sikutaka kutangulia kumtumia Mustafa sms. Nilitaka aanze yeye. Lakini hakutuma wala hakunipia simu. Nikakasirika. Ilipofika saa tisa ndipo nilipoona sms yake.

“Mambo?” Akaniuliza.

Na mimi nikamuandikia kumjibu.

“Poa. Vipi?”

“Poa tu. Mambo yanakwendaje?” Akanitumia tena.

Nikatamani kusikia sauti yake. Nikamuandikia.

“Nipigie.”

Salio nilikuwa nalo lakini sikutaka kupiga mimi.

Baada ya muda kidogo akanipigia. Nikaipokea simu yake.

“Hello!”

“Helo baby. Uko wapi?” Akaniuliza.

“Niko nyumbani.”

“Unaweza kuja hapa…” Alitaja jina la hoteli fulani ambayo sikufahamu ilikuwa wapi.

“Sipafahamu,” nikamwambia.

“Mwambie mwenye teksi yeyote atakuleta.”

“Unataka nije muda huu?”

“Ndiyo.”

“Subiri basi nijitayarishe.”

“Ukiwa tayari nijulishe.’

“Sawa.”

Mustafa akakata simu.

Nikaanza kujitayarisha. Mpaka saa kumi nikawa tayari. Nikatoka na kufunga mlango wangu kisha nikaenda kukodi teksi. Teksi ikanipeleka kwenye hiyo hoteli iliyokuwa Ubungo.

Niliposhuka kwenye teksi nikampigia simu Mustafa. Mustafa alipopokea simu nikamuuliza.

“Uko na nani?”

“Niko mwenyewe. Amina yuko na Shabir.”

“Wao si wako kwenye ile hoteli nyingine.”

“Ndio wao wako kule.”

“Usiwaambie kuwa umeniita hapa.”

“Kwani wewe uko wapi?”

“Nimeshafika, niko hapa nje ya hoteli.”

“Ingia.”

“Hapana, nifuate.”

“Subiri nakuja.”

Baada ya muda kidogo Mustafa akatoka nje ya hoteli. Alionekana wazi kuwa alikuwa ameanza kulewa.

“Mishi vipi?” Akaniuliza.

“Poa,” nilimjibu nikiwa na hofu kidogo.

“Twende.”

Akanishika mkono tukaingie mle hotelini. Kama Mustafa angenitazama vizuri angegundua kuwa nilikuwa na wasiwasi na sikuwa nikijiamini lakini nilikuwa nikijikaza tu kwa sababu nilishaamua kuwa naye.

Mustafa alikuwa ameanza kunywa pombe tangu saa tisa. Akaanza kunishawishi na mimi nilewe.

“Si nimekwambia situmii pombe,” nikamwambia.

“Sasa itakuwaje wakati mimi nakunywa pombe, itabidi na wewe unywe.” Mustafa akaniambia kwa sauti ya kilevi.

“Siwezi kunywa, sijazoea.”

“Ndiyo ujizoeshe sasa.”

“Nitaanza siku nyingine, si leo.”

“Nitakuchanganyia na soda, kunywa kidogo.”

“Hapana bwana, niache tu.”

“Kula kuku basi.”

“Kuku nitakula.”

Mustafa akaniagizia kuku mzima na soda. Nilimla mpaka kijasho chembamba kilinitoka. Pamoja na hamu ya nyama ya kuku niliyokuwa nayo nilimbakisha. Si kwa sababu ya kuigiza tabia za watu wanaokula katika mahoteli makubwa na kubakisha vyakula hata kama hawajashiba, mimi nilibakiza kwa sababu nilishiba.

Karibu nusu ya kuku huyo aliondolewa na kwenda kutupwa.

Wakati huo wote, tulikuwa tukiendelea na mazungumzo na Mustafa. Mazungumzo yetu yalikuwa yakikatizwa mara kwa mara kwa sababu simu ya Mustafa, ilikuwa inapigwa sana. Mazungumzo yake makubwa na wenzake hao yalikuwa ni ya biashara. Kulikuwa na kipindi alipigiwa simu na Shabir.

Shabir alimuuliza.

“Uko wapi?”

Mustafa akamtajia hoteli tuliyokuwa. Nilipata wasiwasi sana kuwa Shabir angeweza kufika pale na kuniona. Mimi sikutaka Shabir wala Amina aujue uhusiano wangu na Mustafa. Ingekuwa ni aibu wakijua kwa vile Amina anajua kuwa nina mume.

Mustafa alipoirudisha simu kwenye mfuko wa shati lake nilimuuliza.

“Ni Shabir?”

“Ndio Shabir.” Akanijibu kwa mkato.

“Amekwambia anakuja?”

“Hapana, hatakuja. Yuko na rafiki yako.”

“Mimi sitaki wajue mapema kuwa uko na mimi.”

Inaendelea...

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST