HADITHI: Bomu Mkononi - 11

3 months ago 53

By  Faki Faki

Mwananchi Communications Limited

“JITAHIDI mwenzangu uje ujenge nyumba yako.”

Siku zote hizo nilikuwa natamani sana kumuona huyo mwanamme wa Amina. Siku moja Musa akiwa safarini, Amina alinipigia simu akaniambia walikuwa katika hoteli kubwa pale Ubungo, yeye na bwana wake na wangekuwa hapo kwa siku mbili.

“Nialike basi nije nimuone shemeji,” nikamwambia.

“Njoo tu, utamuona.”

“Nije sasa hivi?” Nikamuuliza.

“Kwani mume wako hayuko?”

“Yuko safarini.”

“Basi njoo tu. Kodi teksi nitakuja kuilipia mimi.”

“Sawa, basi najitayarisha nije.”

“Ukiwa tayari njoo tu, ukifika nipigie simu unijulishe.”

“Sawa.”

Amina akakata simu.

Tamaa ya pesa alizokuwa akipata mwenzangu ilinifanya niwe mpuuzi. Na siku ile ndio niliyoanza kukosa uaminifu kwa Musa, kuondoka nyumbani kwenda sehemu ya starehe bila ruhusa yake.

Baada ya saa moja nikawa nimeshajitayarisha nikatoka na kufunga mlango wa mbele. Nilikodi teksi kama alivyoniambia Amina ikanishusha Ubungo mbele ya hoteli hiyo.

Nikatoa simu na kumpigia Amina.

“Nimeshafika,” nikamwambia.

“Uko kwa wapi?” Amina akaniuliza.

“Niko nje ya hoteli.”

“Nisubiri karibu na mlango nakufuata.”

Baada ya robo saa hivi nikamuona Amina ametokea kwenye mlango wa hoteli hiyo, akaangaza macho yake huku na huku kunitafuta. Nikamfuata.

Wakati namfuata aliniona akatabasamu.

“Shoga umependeza!” Akaniambia.

“Asante.”

Siku ile nilipendeza kweli. Nilikuwa nimevaa kihuni kwa vile mume wangu hakuwepo na nilikuwa nakwenda kwenye hoteli kubwa. Nilitaka huyo shemeji akiniona ajue kuwa nilikuwa msichana wa kisasa pengine kumzidi hata Amina.

Vile nilivyokuwa nimevaa, kama Musa anatokea na kunioana tena nikiwa katika hoteli kama ile, moja kwa moja angejua nilikwenda kujiuza na angenipa talaka yangu hapo hapo.

Yale mafunzo ya kungwi wangu nilikuwa nimeyasahau kabisa.

Amina akanishika mkono kiushosti tukaingia ndani ya hoteli. Ilikuwa hoteli ya kifahari iliyokuwa imejaa wazungu. Sikuwahi kuingia katika hoteli kama ile. Hoteli nilizokuwa ninakwenda na Musa zilikuwa za kawaida tu.

Nikamuonea wivu mwenzangu kwa kupata bwana mwenye uwezo na kufanya naye matanuzi ya hali ya juu.

Amina akanipeleka  katika ukumbi wa hoteli ambako nilimkuta mwanamme wake akinywa kilevi cha gharama. Amina alikuwa hatumii kilevi lakini yule mwanamme alimfanya naye aanze kulewa.

Kwenye meza nilikuta chupa mbili. Moja upande wa shemeji na nyingine upande wa Amina. Ile iliyokuwa upande wa Amina niliisoma, ilikuwa Reds.

“Kutana na shemeji yako.” Amina akaniambia.

Jamaa mwenyewe alikuwa kama chotara. Alikuwa na mwili mdogo sana lakini alivaa vizuri na kupendeza. Alikuwa amekata ndevu zake vizuri na kuonekana mtu makini sana.

Mtu huyo aliinua uso akanitazama.

“Karibu,” akaniambia huku akitabasamu.

 “Asante. Habari yako.” Nikamsalimia.

“Nzuri. Hujambo?” Na yeye akanisalimia.

“Nashukuru niko poa.”

Nilivuta kiti na kuketi. Amina naye aliketi.

“Shabir. Huyo ni shemeji yako wa ukweli anaitwa Mishi.” Amina alimwambia mwanaume wake.

Jamaa huyo alitingisha kichwa chake kumkubalia.

“Nimefurahi kumuona,” akasema kisha akanitazama.

“Karibu sana Mishi. Mimi naitwa Shabir.”

“Nimefurahi kukuona na kukufahamu shem wangu.”

“Tangu tukiwa watoto tulikuwa pamoja. Siri yake, siri yangu.” Amina akamwambia mwanaume wake.

“Namuona amependeza sana.” Shabir akasema huku akinitazama tazama.

“Unatumia kinywaji gani Mishi?” Akaniuliza.

“Mh! Labda soda tu.”

“Kwanini unywe soda wakati vinywaji vingine vipo.” Shabir akaniuliza.

“Situmii ulevi wa aina yoyote.”

“Utakunywa soda gani?” Amina aliniuliza.

“Cocacola.”

Amina akamuita muhudumu na kumuagizia soda ya Cocacola moja.

Wakati tunasubiri niletewe soda mazungumzo yalikuwa yanaendelea.

 “Shem utakuwa hapa Dar hadi lini?” Nikamuuliza Shabir.

“Mimi nipo kwa kipindi kirefu.” Shabir akanijibu.

“Si unasafiri nje kibiashara?”

“Ndio lakini kwa sasa kuna mtu namtumia, anakwenda yeye badala yangu. Mimi napumzika kidogo. Mama yangu ni mgonjwa. Nilirudi jana kutoka Arusha.”

“Kumbe mama yuko Arusha.”

“Mimi mwenyewe pia ni mzaliwa wa Arusha. Hapa Dar nakuja kikazi tu.”

“Nimekuelewa. Lakini ulipoondoka Arusha hali ya mama ikoje?”

“Hajambo kidogo.”

Mhudumu akaniletea soda. Aliweka chupa juu ya meza akafungua kizibo kisha akanimiminia kwenye bilauri.

Niliinua bilauri nikaipiga funda soda iliyokuwa inachemka kwa gesi.

Hapo hapo simu ya bei mbaya ya Shabir iliyokuwa juu ya meza ikaita. Shabir aliitupia macho kisha akaishika na kuipokea.

“Mustafa, niambie…” Akasema.

Alisikiliza kwa karibu nusu dakika kisha akasema.

“Mimi niko hapa.” Alitaja jina la hoteli tuliyokuwa kisha akaongeza.

“Unaweza kuja muda huu?”

Alisikiliza tena kidogo kisha akauliza.

“Unakuja sasa hivi…okey…”

Akairudisha simu juu ya meza.

“Ni nani?” Amina akamuuliza.

“Ni rafiki yangu Mustafa, alikuwa anataka kujua niko wapi.” Shabir akamjibu.

“Ndiye huyo uliyesema unafanya biashara naye?’ Na mimi nikamuuliza.

“Ndiye yeye. Yeye anaishi hapa hapa Dar. Alirudi juzi kutoka India.”

Kwa vile umbea ulikuwa umenishika nikamuuliza tena.

“Alileta nini?”

“Alileta pikipiki. Nilikuwa na oda ya pikipiki mia mbili.”

Hatukukaa kwa muda mrefu Mustafa akatokea. Kidogo alikuwa amemzidi umri Shabir. Alionekana kijana mtanashati aliyenyoa nywele zake vizuri na kuziweka ndevu zake vyema.

Alipofika alitusalimia akavuta kiti na kuketi.

Bila shaka alikuwa akifahamiana vizuri na Amina kwani Amina ndiye aliyemtambulisha kwangu.

Na yeye aliagiza soda kama mimi. Sikujua kama alikuwa hatumii kilevi au alikuwa ameamua tu kwa sababu zake mwenyewe. Tukawaacha wakizungumza na Shabir. Na mimi na Amina tukawa tunazungumza yetu.

Jua lilipokuwa linakuchwa nikamwambia Amina kuwa ninarudi nyumbani.

Wakati ule namuaga Amina nikamuona Mustafa ameinuka.

“Unaondoka?” Amina akamuuliza.

“Ndio, nataka kwenda nyumbani nioge nibadili nguo. Nilikuwa Kibaha tangu asubuhi.”

“Basi utampa lifti shoga yangu, umuache nyumbani kwake.”

“Hakuna tatizo. Twende Mishi.” Mustafa akaniambia kwa furaha.

Nikanyanyuka kwenye kiti na kumuaga Shabir.

“Shabir kwaheri, tutaonana siku nyingine,” nilimwambia.

“Usijali, tutaonana.” Shabir akaniambia.

Nikaondoka na Mustafa. Tukiwa nje ya hoteli Mustafa alinipakia kwenye gari lake. Alikuwa na gari jipya aina ya Range Rover la rangi nyekundu.

Akaliwasha gari tukaondoka.

“Unaishi wapi?” Akaniuliza mara tu alipoliondoa gari.

“Naishi Kimara Baruti.”

“Unafanya kazi wapi Mishi?”

Hapo nilisita kumjibu ukweli kwa vile sikuwa na kazi na nilikuwa nimeolewa. Nikaishia kumuuliza.

“Mimi…?”

“Si ndiyo.”

“Niko nyumbani tu.”

“Uko na wazazi wako?”

Ilibidi nimkubalie.

“Ndiyo, bado naishi na wazazi.”

“Unaonaje tukiwa marafiki?”

Moyo wangu ulishituka ingawa nilitarajia kuwa angeniambia hivyo.

Uso wangu ukawa umepatwa na tabasamu la fadhaa.

“Si tumeshafahamiana?” Nikajidai kumuuliza.

“Kufahamiana tu haitoshi, nataka tuwe marafiuki kabisa.”

Mustafa aliponiona nimesita nikifikiria kumkubalia au kumkatalia alianza kunimwagia sera.

“Unajua nilipokuona pale hotelini moyo wangu ulishituka sana ndio maana nilipoona unamuaga shoga yako na mimi nikainuka haraka. Nilikuwa nataka nipate nafsi ya kuzungumza na wewe.”

“Nilikuona na nilijua ulikuwa na jambo.”

Mustafa akacheka

“Kumbe ulishanisoma?”

“Sasa kitu gani kilichokuvutia?” Nikamuuliza kwa kuzuga.

“Ni wewe mwenyewe jinsi ulivyo.” Mustafa alinijibu haraka kama vile jibu hilo lilikuwa midomoni mwake.

“Nikoje?”

“Mishi unauliza jibu? Au una bwana anakupa pesa nyingi?”

Inaendelea...

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST