By Faki Faki
Mwananchi Communications Limited
ALINIULIZA jina langu. Nilipomtajia jina langu akaniuliza tena.
“Leo ni siku ya harusi yako, je umekubali kuolewa na Musa?”
“Nimekubali.” Nikamjibu.
Nilipomjibu hivyo sheikh huyo akatoka. Tukakaa hadi saa mbili na nusu. Nikasikia vigelegele huko nje. Nikajua mambo yalikuwa tayari. Haukupita muda mrefu Musa na yule sheikh pamoja na mtu mwingine ambaye sikumfahamu wakaingia mle chumbani.
“Mpe mkono mke wako.” Sheikh akamwambia Musa.
Musa akanipa mkono. Wakati mikono yetu imeshikana, sheikh alituombea dua ndefu.
Alipomaliaza kutuombea dua alituambia.
“Bwana Musa na Bi Mishi hivi sasa ni mume na mke. Muishi kwa amani jamani. Kama ambavyo mmeoana kwa wema ikilazimika kuachana muachane kwa wema.”
“Tumekuelewa sheikh.” Musa akamwambia huku akiketi kitandani kando yangu.
Kulikuwa na mpiga picha ambaye alikuwa amekazana kutupiga picha. Baadhi ya wanawake walikuwa wameingia mle chumbani wakipiga vigelegele.
Yule sheikh baada ya kutupa nasaha zake aliondoka akaacha wanawake waking’ara mle chumbani. Baadaye kungwi wangu aliwafukuza mle chumbani akawaambia wakapige vigelegele vyao huko nje.
Picha ziliendelea kupigwa. Tulipiga picha na ndugu, jamaa na marafiki walioingia mle chumbani kutupongeza. Miongoni mwa watu tuliopiga nao picha alikuwa shangazi yangu, kungwi wangu na Amina.
Baada ya hapo tulikula kombe. Unalijua kombe? Kombe ni chakula walichoandaliwa bwana na bibi harusi. Kwa sababu ya kiherehere hatukula sana. Chakula tulikibakisha.
Musa akazungumza na kungwi wangu. Walichokizungumza sikukisikia lakini baada ya hapo mume wangu akanishika mkono na kuniinua.
“Tunaondoka,” akaniambia.
Tukatoka. Nilikuwa mimi, mume wangu, kungwi na Amina pamoja na wanawake wengine wasiopungua watano.
Huko nje tulipakiwa kwenye magari mawili. Gari moja tulipanda mimi, mume wangu, kungwi wangu na Amina. Gari la pili walijipakia wanawake wengine. Tukaelekea Kimara nyumbani kwa Musa.
Tuliacha sherehe zikiendelea. Tulipofika Kimara tuliingia nyumbani. Sebule ilikuwa imepambwa vizuri. Tukakaa sebuleni.
Baadaye mimi na mume wangu tukaingia chumbani kupumzika. Ulikuwa usiku niliojisikia furaha sana.
Kwa kufupisha maneno ni kwamba wageni wote waliofika waliondoka akabaki kungwi wangu na Amina. Walikaa kwangu kwa siku saba wakinisaidia kazi za nyumbani. Mimi mwenyewe nilikuwa sifanyi kazi yoyote. Baada ya hizo siku saba ndipo kungwi akaniambia.
“Tunakuachia nyumba yako, hivi sasa unaweza kutoka kufanya kazi zako. Sisi tunondoka.”
Nikaachwa na mume wangu. Siku ile ambayo wageni wangu wanaondoka, siku ya pili yake Musa akasafiri kwenda Burundi. Nilichukia kweli kweli. Nilikuwa nataka niendelee kuwa naye. Akaniachia upweke.
Aliondoka saa tatu asubuhi nikamsindikiza hadi nje.
“Uende salama,” nikamwambia huku nikijikaza nisionyeshe majonzi niliyokuwa nayo.
“Na wewe ubaki salama.” Na yeye akaniambia. Usoni kwake sikuona kama alikuwa na huzuni kama mimi.
Baada ya kuagana naye akaondoka. Siku ile mchana kutwa tulikuwa tunawasiliana. Kama sitapiga mimi simu, atapiga yeye kunijulisha mahali walipofika. Ilikwa ni kila baada ya saa chache tulipigiana simu.
Nakumbuka walipofika mpakani ndio walikaa sana. Aliniambia kuwa walikuta mlolongo mrefu wa magari. Kwa vile niliwahi kusikia kuwa maderava wakifika hapo huwaachia magari mataniboi wao na wao kwenda kulala na wasichana, usiku kucha kila nilipoamka nilikuwa nampigia simu ili nijue kama kalala na mwanamke.
Mimi mwenyewe pia nilipata shida kulala peke yangu lakini nilijikaza kwa vile sikuwa na la kufanya. Nilikuwa nikiwaza labda wezi watakuja kuvunja wakijua kuwa mume wangu hakuwepo. Nikajiuliza nitafanyaje kama mlango utavunjwa wakati nilikuwa peke yangu nyumbani?
Lakini mawazo hayo yalinijia siku za mwanzo mwanzo tu, baadaye nikazoea. Hata kule kumpigia simu Musa kukapungua kadiri siku zilivyozidi kwenda.
Mwisho nikawa nampigia mara moja tu kwa siku hasa pale aliponijulisha kuwa alikuwa ameshafika Burundi.
Musa alikaa wiki nne ndipo akarudi. Wakati tunazungumza kwenye simu aliniambia wiki mbili alizipitisha wakiwa mpakani wakati wa kwenda na wakati wa kurudi kutokana na milolongo mirefu ya malori ya usafirishaji, yanayotoka na yanayokwenda Burundi.
Siku aliyorudi nyumbani ilikuwa furaha kweli kweli. Musa alileta kuku, magunia mawili ya mkaa, gunia moja la mchele na pia alikuwa ameninunulia nguo na viatu kutoka Burundi.
Maisha yangu na Musa yalianza kwa upendo na furaha. Siku ambayo Musa alikuwa na mapumziko alikuwa akishinda nyumbani na kila wiki alikuwa akinitoa mara mbili kwenda kwenye matanuzi.
Siku ambayo alisafiri ndiyo siku iliyokuwa na majonzi kwa upande wangu. Nilikuwa nimemzoea Musa na sikupenda nimkose.
Kwa vile moyo wangu ulikuwa na wasiwasi wakati wote Musa akisafiri, kulikuwa na siku nikamuuliza.
“Hivi unajisikiaje unaponiacha mimi na kusafiri kwa mwezi mzima?”
“Najisikia kawaida tu, si nimeshazoea.” Musa akanijibu.
“Unajisikia kawaida, unakaa mwezi mzima bila kukutana na mke wako?”
“Kwani wewe unafikiriaje?”
“Nafikiria kwamba kunakuwa na michepuko mingi huko njiani unakokwenda ndio sababu unasema unaona kawaida tu.”
“Eh! Naona leo umeanza kunishutumu! Umefikiria nini mpaka ukaniambia hivyo?”
“Nimefikiria hivyo nilivyokwambia lakini nimekwambia kwa nia njema kwa vile tabia za madereva wa malori zinaeleweka. Sikulaumu kwa sababu unakaa muda mrefu bila mke wako na wewe ni mwanaume, unaweza kutamani.”
“Hapana mke wangu. Sijatamani mwanamke yoyote tangu nilipoanza kuwa na wewe.”
“Nilichokuwa nimekusudia kukwambia ni kuwa ni muhimu kujizuia lakini pale unaposhindwa kabisa basi tumia kinga.”
Musa akatikisa kichwa kusikitika. Ingawa hakutamka neno lakini kilichomsikitisha nilikijua. Ni lile funzo langu kwamba endapo atashindwa kujizuia atumie kinga. Lilikuwa funzo zuri lakini linalofedhehesha, ndio sababu Musa alisikitika.
“Kwanini leo umeamua kuniambia hivyo?” Akaniuliza.
“Usifikiri kuna tatizo, tunakumbushana tu. Waswahili wanasema. ‘Mwenda pwani mwambie akirudi.’ lakini mimi nakwambia wakati unakwenda. Bora ya nusu shari kuliko shari kamili. Ukitembea na mwanamke itakuwa nusu shari, ukipata ukimwi itakuwa shari kamili kwa maana ukimwi huo hutaupata wewe tu nitaupata na mimi.”
Musa akashusha pumzi ndefu.
“Nimekuelewa mke wangu lakini naomba uniamini sitakusaliti hata siku moja,” akaniambia kwa uso wa huzuni.
“Mimi pia niamini, sitakusaliti hata siku moja.”
Ili kumfariji Musa niliyemuona amefadhaika kwa kupata hisia kuwa namshutumu, nilimkumbatia kisha nikamshumu. Wakati akiwa kifuani kwangu nilimuhisi akipumua kwa nguvu na moyo wake ulikuwa unakwenda mbio.
Nikamuonea huruma lakini nilijua ujumbe wangu ulikuwa umefika kwani baadhi ya madereva wa malori hawaaminiki. Kwa hiyo nilimwambia kusudi ili aweke tahadhari.
Siku ile nilimuonya mwenzangu, mimi mwenyewe nilisahau kujionya na pia sikupata mtu wa kunionya. Amina alikuwa na tabia ya kunitembelea nyumbani mara kwa mara. Siku ambazo Musa alikuwa safarini, humuita na kulala naye hadi siku ambayo Musa ananiarifu kuwa anarudi.
Kulikuwa na siku Amina aliniambia alipata bwana mfanyabiashara ambaye huzunguka katika nchi mbalimbali za Kiasia. Alikuwa akimletea zawadi mbalimbali zikiwamo nguo na vitu vingine vingine vya thamani.
Katika kipindi cha miezi miwili tangu Amina ampate bwana huyo alibadilika sana. Alikuwa akibadili nguo kila wakati na pesa ilikuwa haimsumbui. Kila alipopewa pesa Amina alikuwa akija nyumbani kunitambia.
“Jana nimelala naye kanipa milioni mbili,” aliniambia.
“Wacha we!”
“Huamini, ngoja nikuonyeshe.”
Amina alifungua mkoba wake na kunuonyesha vitita vya noti nyekundu.
“Huyo bwana umshike sana, ukimponyosha tu wenzako watamchukua.”
“Si rahisi, nimemuweka hapa.” Amina aliniambia huku akinionyesha kiganja chake alichokikunja kama anapokea kitu.
“Nigawie na mie japokuwa laki moja rafiki yangu.”
Amina akafungua mkoba wake akatoa shilingi laki moja na kunipa.
“Nimefungua akaunti mwenzako. Hivi sasa nina karibu shilingi milioni sita. Nataka niziweke ili nije ninunue kiwanja.”
Inaendelea...