Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia, ASEAN nchini Laos.
11 Oktoba 2024 Amani na Usalama
Akiwa ziarani nchini Laos, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo Oktoba 11 ameshiriki katika ufunguzi wa mkutano wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia, ASEAN, akiangazia kuwa ushirikiano wa jumuiya hiyo ya kikanda na Umoja wa Mataifa umeimarika zaidi.
António Guterres amesema anashukuru hasa kwa mchango muhimu wa wanachama wa ASEAN katika operesheni za kulinda amani. Ameonesha "mshikamano kamili" na walinda amani wawili wa Indonesia, ambao wanahudumu nchini Lebanon na walijeruhiwa na mashambulizi ya Israeli.
Mtandao
Akirejelea Mkataba wa Zama Zijazo uliopitishwa katika Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka huu 2024, Guterres ameangazia maeneo makuu manne ya ushirikiano ambayo yanawezesha "matarajio".
Ya kwanza ya haya ni mtandao. Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa kote Asia ya Kusini-Mashariki, upatikanaji wa ‘broadband’ na mtandao wa simu umeongezeka sana. Hata hivyo, "mgawanyiko wa kidijitali unaendelea."
Kulingana na yeye, mgawanyiko wa akili wa mnemba pia unaundwa. Ili kuzuia mchakato huu, katibu mkuu amesema kuwa nchi zote lazima ziwe na uwezo wa kupata na kufaidika na teknolojia hizi. Kwa kuongeza, mataifa yote lazima yashiriki katika uamuzi juu ya utawala wa Akili Mnemba (AI).
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akutana na mkulima wa kahawa Phuerp (kushoto).
Ufadhili
Jambo la pili alilozungumzia Guterres katika hotuba yake kwa viongozi wa ASEAN ilikuwa ni fedha. Amesema kuwa mageuzi ya usanifu wa fedha wa kimataifa yanahitajika ili kuziba pengo la ufadhili wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.
Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ameangazia baadhi ya mapendekezo yaliyomo katika Mkataba wa Baadaye ili "kuhakikisha kwamba nchi zinaweza kukopa kwa uendelevu" ili kuwekeza katika maendeleo yao ya muda mrefu.
Tabianchi
Tabianchi ilikuwa kipaumbele cha tatu kilichotajwa na mkuu wa Umoja wa Mataifa. Amesisitiza kuwa nchi za ASEAN "zinakabiliwa na vurugu ya tabianchi," ambazo zinajidhihirisha katika majanga kama vile Super Typhoon Yagi. Kimbunga hicho cha kitropiki kiliathiri Ufilipino, Uchina na Vietnam mapema Septemba 2024.
Guterres amekumbushia kuwa kufikia mwaka ujao, nchi zote lazima zitoe Michango Mipya Iliyoamuliwa Kitaifa, inayowiana na kupunguza ongezeko la joto duniani hadi 1.5°C.
Amani na Usalama
Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amekiri jukumu muhimu la ASEAN katika kuendelea kutafuta mazungumzo na njia za amani za kutatua mizozo kutoka Peninsula ya Korea hadi Bahari ya Kusini ya China.
Hata hivyo, amebainisha kuwa Myanmar inasalia kwenye njia inayozidi kuwa ngumu, huku ghasia na mahitaji ya kibinadamu yakiongezeka.
Katibu Mkuu ametoa wito kwa nchi zote kuongeza ushawishi wao kwa suluhisho la kisiasa la mzozo huo na kutoa mustakabali wa amani ambao watu wa Mynmar wanastahili.
Guterres amehitimisha kwa kusema kwamba katika ulimwengu wa mgawanyiko wa kijiografia unaokua, wenye athari kubwa kwa amani, usalama na maendeleo endelevu, ASEAN ni "wajenzi wa daraja na mjumbe wa amani."