Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada, OCHA, takriban watu milioni 1.9 – sawa na watu tisa kati ya 10 huko Gaza – wamelazimishwa kukimbia makwao kwa nguvu tangu Oktoba 7, 2023 ikiwa ni pamoja na watu ambao wamekuwa wakikimbia mara kwa mara.
Kwa mashirika mengine ya misaada ya Umoja wa Mataifa, “uhaba wa mafuta unaendelea kudhoofisha shughuli za kibinadamu na kuhatarisha utendaji wa vituo vya afya, maji na chakula,” kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia wakimbizi wa Palestina, UNRWA.
Kwa mujibu wa jedwali linaloonesha upatikanaji wa misaada kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa, ni malori 24 pekee yaliyobeba misaada ya kibinadamu iliyoshughulikiwa na kuchukuliwa na UNRWA – ambaye ndio shirika kubwa zaidi la Umoja wa Mataifa linalofanya kazi Gaza – malori hayo yaliingia Ukanda huo kupitia mpaka wa Kerem Shalom kusini mwa Gaza siku ya Jumapili.
Hakuna aliyeingia katika eneo hilo siku ya Jumamosi lakini malori 46 yalifika kaskazini mwa Gaza siku ya Jumamosi kupitia kivuko cha Western Erez.
Ikilinganishwa na mwezi Juni, ambapo karibu malori 1,300 yaliingia Gaza, jumla ya malori yaliyoingia mpaka sasa kwa mwezi huu wa Julai ni 674 tu, huku ikiwa imebaki wiki moja tu hadi kufika mwisho wa mwezi.
Uingizaji mdogo wa mafuta
Ikilinukuu OCHA, UNRWA lilisema kuwa kati ya tarehe 1 na 21 Julai, zaidi ya lita milioni 2.1 za mafuta ziliingia Gaza, zikiwemo 378,700 mnamo Julai 21 pekee. Hii ni takriban lita 103,000 za mafuta kwa siku, au robo ya lita 400,000 za mafuta ambazo wadau wanakadiria zinahitajika kila siku ili kuendeleza shughuli za kibinadamu huko Gaza.
Changamoto kadhaa zinazoendelea zinazuia ukusanyaji wa misaada ya kibinadamu inayohitajika kutoka kivuko cha Kerem Shalom kusini mwa Gaza, UNRWA imesema huku likieleza kuna uvunjivu sheria na utulivu, miongoni mwa mambo mengine.
Uharibifu wa barabara, majengo na miundombinu kutokana na kuongezeka kwa vurugu huko Jenin, katika Ukingo wa Magharibi.
Hali si hali Ukingo wa Magharibi
Katika tukio linalohusiana na hilo, mtaalam huru wa haki za binadamu amesema hii leo kwamba mamlaka ya Israeli "inaendelea kuwalenga watetezi wa haki za binadamu" katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na walowezi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, na kutoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa watetezi wawili wa haki za binadamu wa kipalestina ambao wamewekwa "kizuizini kwasababu za kiutawala".
Mtaalamu huyo huru Mary Lawlor ambaye aliteuliwa na Baraza la haki za binadamu na sio mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa, kupitia taarifa yake iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu amewataja wanaharakati hao wawili kuwa ni Omar al-Khatib na Diala Ayesh ambao anasema walikamatwa kati ya mwezi Oktoba 2023 na Machi 2024.
Taarifa yake hiyo imeeleza kuwa Bw. al-Khatib anafanya kampeni dhidi ya familia za wapalestina wanaolazimishwa kuondoka katika maeneo kwa lazima kutoka kitongoji cha Jerusalem cha Sheikh Jarrah, wakati Bi Ayesh ni wakili wa haki za binadamu ambaye anaandika na kuweka kumbukumbu za wapalestina wanaofungwa au kuwekwa vizuizini nchini Israel.
Wao na wanaharakati wengine watatu "iliripotiwa kupigwa makofi, kudhalilishwa, kuhamishwa kutoka jela moja hadi nyingine katika muda wa siku moja au mbili, na kulazimishwa kutia saini hati iliyoandikwa kwa lugha ya Kiebrania ambayo hawakuweza kuelewa", alisema Bi Lawlor.
“Watetezi wote watano wa haki za binadamu walikamatwa bila hati. Hawakupewa sababu yoyote ya kwa nini waliwekwa kizuizini. Wote walihojiwa bila kuwepo wakili. Hawakuruhusiwa kuwasiliana na familia zao,” Bi Lawlor alisema.
Vifo na uharibifu
Tukisalia na Ukingo wa Magharibi, ripoti za vyombo vya habari zimeonesha kuwa Wapalestina wanne waliuawa hapo jana siku ya Jumanne.
Magari ya kivita ya wanajeshi wa Israel wameripotiwa kuingia Qalandiya - kambi ya wakimbizi iliyojaa watu wengi kaskazini mwa Jerusalem - na kuharibu nyumba ya Mpalestina anayedaiwa kufanya shambulizi dhidi ya Israeli.
Kuongezeka kwa uhasama katika Ukanda wa Gaza kunaleta maafa makubwa kwa watoto.
Taarifa za hivi karibuni kutoka OCHA ziliripoti kwamba Wapalestina 554 wameuawa kati ya 7 Oktoba 2023 na 15 Julai 2024, wakati Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF imeeleza kuwa watoto 143 wamekufa katika Ukingo wa Magharibi ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki tangu Oktoba 7, kwa wastani mtoto mmoja huuawa kila baada ya siku mbili.
Wahanga wa kipalestina ni pamoja na watu 539 waliouawa na vikosi vya Israeli, 10 na walowezi wa Israeli na saba ambao wahusika wao walikuwa vikosi vya Israeli au walowezi.
Katika kipindi hicho, Waisraeli 14 (wanajeshi tisa wa Israel na walowezi watano) waliuawa na Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi. Huko Israel, mashambulizi ya Wapalestina kutoka Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yamegharimu maisha ya Waisraeli wanane na Wapalestina wanne.
Kati ya tarehe 15 na 21 Julai UNRWA iliripoti angalau oparesheni 169 za vikosi vya usalama vya Israeli (ISF) zilirekodiwa katika Ukingo wa Magharibi. "Zaidi ya Wapalestina 110 ... waliwekwa vizuinini na ISF katika kipindi hicho na kulikuwa na Wapalestina watatu waliorekodiwa kuuawa.
"Mtu mmoja aliuawa wakati wa operesheni ya ISF huko Beit Ummar, kusini mwa Ukingo wa Magharibi, tarehe 19 Julai," UNRWA ilisema.
Vurugu kufuatia tamko la ICJ
Kwa mujibu wa UNRWA tarehe 15 Julai, ISF ilibomoa nyumba tano katika kijiji cha Al Walajah, kaskazini mwa Bethlehem, na kusababisha wakimbizi wanaokadiriwa kufikia 39 wa Kipalestina kuhama makazi yao.
Na kufuatia kutolewa kwa maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) tarehe 19 Julai, mashambulizi ya walowezi wa Israel yaliripotiwa kutekelezwa dhidi ya jamii za Wapalestina huko Huwwara na Burin, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, na huko Masafer Yatta, kusini Magharibi.
Tamko hilo la mahakama limeeleza kuendelea kuwepo kwa Israel katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu "ni kinyume cha sheria" na kwamba "Nchi zote ziko chini ya wajibu wa kutotambua" uvamizi huo wa miongo kadhaa, lilifuatia ombi la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu athari za kisheria zinazotokana na sera na desturi za Israel katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, ikiwemo Jerusalem Mashariki.
Takwimu za hivi karibuni zilizokusanywa na OCHA kuhusu ubomoaji na kuwahamisha katika Ukingo wa Magharibi zilionesha zaidi ya ubomoaji wa majengo 820 yanayomilikiwa na Wapalestina katika eneo hilo tangu mwanzoni mwa mwaka.
Kwa kiwango cha sasa cha uharibifu, rekodi ya majengo 1,400 yameharibiwa hadi kufikia mwisho wa mwaka, na kupita kiwango cha juu cha hapo awali cha majengo 1,177 mwaka 2023 na majengo 1,094 mwaka 2016.