Wapalestina waliokimbia makazi yao wanasimama kwenye foleni kwenye usambazaji wa chakula kaskazini mwa Gaza (Maktaba)

25 Julai 2024 Msaada wa Kibinadamu

Wakati Rais wa Marekani Joe Biden akijiandaa kukutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hii leo nchini Marekani ambapo wanatarajia kujadili maendeleo ya kusitisha mapigano huko Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa mateka wote ambao bado wanashikiliwa katika eneo hilo, hali ya njaa na utapiamlo imeendelea kuwakumba Wanagaza, huku mashirika ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa yakionya kwamba hakuna kilimo cha eneo kubwa wala bustani kinachofanyika sabab ya ukosefu wa usalama.

Wakati hayo yakijiri, ripoti za vyombo vya habari mbalimbali zinaonesha kuwa mazungumzo ya amani na kubadilishana mateka huko Doha yaliyopangwa kufanyika leo Alhamisi nchini Qatar yameahirishwa hadi mapema wiki ijayo. Takriban mateka 116 bado hawajulikani walipo, huku 44 wakiaminika kufariki, ripoti zinasema, karibu miezi 10 tangu mashambulizi yanayoongozwa na Hamas katika maeneo mengi kusini mwa Israel yaliposababisha vifo vya watu 1,250 na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka.

Tahmini ya viwango vya njaa huko Gaza iliyotolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada, OCHA, ilionya kwa mara nyingine tena kwamba unafuu mdogo sana unawafikia watu wanaohitaji zaidi. “Ukosefu wa usalama, barabara zilizoharibika, uvunjaji wa sheria na utulivu, na vikwazo vya kuwafikia wenye uhitaji vinaendelea kutatiza usafiri kwenye njia kuu ya mizigo ya kibinadamu kati ya mipaka ya Kerem Shalom na Khan Younis na Deir al Balah.”

Majiko ya kijamii yapo hatarini

OCHA ilibainisha kuwa usambazaji usitosha wa mafuta na misaada unaoendelea kutoka kati/kusini mwa Gaza hadi kaskazini umesababisha viwanda sita vya kuoka mikate kaskazini mwa Gaza - vinne katika mji wa Gaza na viwili kaskazini mwa Gaza - vikipokea mafuta kiasi kidogo ambacho kimetosha kusaidia wahitaji kwa siku chache.

“Uhaba mkubwa” wa bidhaa umeathiri majiko ya kijamii yanayopika chakula na kutoa kwa wenye uhitaji na kuongeza “hatari ya chakula kuharibika na uvamizi wa chakula” huku kukiwa na joto kali katika msimu huu wa kiangazi.

“Kwa kuongezea, uwezo wa uzalishaji wa chakula cha moto katika majimbo ya Gaza na Kaskazini mwa Gaza haujatosha kusaidia makumi ya maelfu ya watu wapya waliokimbia makazi yao,” OCHA iliendelea kueleza katika taarifa yake, kama ilivyoeleza kuwa “kukosekana kwa bidhaa za kibiashara kaskazini mwa Gaza kwa karibu miezi mitatu kumesababisha ukosefu wa karibu wa vyanzo vya protini kama vile nyama na kuku kwenye soko la ndani.

Kwa sasa kaskazini mwa Gaza, ni aina chache tu za mboga zinazozalishwa nchini humo zinapatikana kwa bei “isiyowezekana kumudu”, shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilieleza, huku likionya kwamba ukosefu wa “mbegu, mbolea na pembejeo nyingine za uzalishaji wa wanyama na mazao” umesalia “kikwazo kikuu” kurejesha uzalishaji wa chakula wa ndani huko Gaza.

OCHA pia ilizungumzia operesheni za kijeshi za Israel ambazo zimeharibu Rafah tangu mwanzoni mwa mwezi Mei na kusababisha msafara wa watu wanaokimbia eneo hilo wiki hii kutoka mashariki mwa Khan Younis, “ambako uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo ulijilimbikizia kabla ya vita”.

Mbali na uharibifu ambao umekwisha fanyoka, mashamba ya Gaza sasa hayajashughulikiwa. “Madhara yake yataonekana zaidi msimu ujao wa kilimo na huenda yakaharibu maisha ya watu,” imeonya taarifa ya OCHA.

Tathmini hiyo inalingana na tahadhari za awali zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO, ambalo lilionesha kuwa kilimo katika Ukanda wa Gaza kinawakilisha zaidi ya asilimia 40 ya eneo la kijamii na kuchangia hadi asilimia 30 ya matumizi ya kila siku.

“Uharibifu wa sekta ya kilimo kutokana na mzozo unaoendelea huko Gaza ni mkubwa, na kusababisha uzalishaji muhimu wa ndani wa chakula kibichi na chenye lishe kukaribia kusimamishwa, na hivyo kupunguza upatikanaji wa vyakula muhimu vinavyohitajika kwa lishe bora,” ilisema sehemu ya taarifa.

Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa ya tathmini ya viwango vya njaa IPC, asilimia 96 ya wakazi wa Gaza - takriban watu milioni 2.15 - wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula katika kiwango cha “mgogoro” au zaidi. Hiyo ni kiwango cha tatu cha faharasa ya Ainisho ya Awamu ya Uhakika wa upatikanaji wa Chakula (IPC).