Wafanyikazi wa afya wakipeleka vifaa vya chanjo ya polio kwenye vituo vya huduma za afya uko Gaza mnamo Septemba 2024.

11 Oktoba 2024 Amani na Usalama

Wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wameendelea kuonya kwamba hali ya raia huko Gaza, inazidi kuwa mbaya, huku jeshi la Israel likianzisha tena harakati zake kuelekea kaskazini ambako takriban watu 400,000 wanakabiliwa na amri ya kuhama.

"Katikati ya wiki iliyopita, jeshi la Israel liliimarisha operesheni kaskazini mwa Gaza, na kulitenga zaidi eneo hilo kutoka sehemu nyingine ya Ukanda wa Gaza na kuhatarisha upya maisha ya raia katika maeneo hayo," amesema Bi. Ravina Shamdasani msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu OHCHR akizungumza leo na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi.

Ameongeza kuwa "Mashambulio makali, mashambulizi ya makombora, ufyatuaji risasi kwa njia ya anga na uvamizi wa ardhini vimetokea katika siku zilizopita, na kugonga majengo ya makazi na vikundi vya watu, na hivyo kusababisha vifo vingi na kwa mara nyingine tena, Wapalestina wengi kulazimika kuhama makwao katika eneo hilo."

Duru ya pili ya chanjo ya polio

Wakati mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa na washirika wake wakijiandaa kuzindua awamu ya pili ya kampeni kubwa ya chanjo ya polio wiki ijayo, Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, Dkt. Rik Peeperkorn, amesisitiza athari za kukosekana kwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo na, hasa, kaskazini.

Amesema "Hospitali nyingi za kaskazini zinakosa mafuta. Operesheni nyingi za Umoja wa Mataifa na za kibinadamu hazifanyiki katika maeneo ya kaskazini. “

Ameendelea kusema kuwa “Hospitali nyingi zinakosa vifaa vichache vya matibabu na tuko mwaka mmoja katika shida hii.”

Dkt Peeperkorn amethibitisha kwamba operesheni tatu za misaada ya kibinadamu kaskazini mwa Wadi Gaza hazijafanikiwa wiki hii.

Kwa mantiki hiyo amesema "Tunaomba tena kwamba operesheni hizi za misaada ya kibinadamu kaskazini, popote, kusini, zinahitaji kufanyika."

Operesheni hiyo ya awamu ya pili ya chanjo itaendeshwa kwa ushirikiano wa WHO, shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na kushirikisha wadau wengine.