Muyisa Kalala Raymond, Mhudumu wa afya kutoka hospitali kuu ya Goma-DRC, ambaye pia ni mmoja wa watu wa kwanza ambao wamepata chanjo dhidi ya ugonjwa wa MPOX jimboni Kivu Kaskazini.
9 Oktoba 2024
Na George Musubao - Goma, DRC
Chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa ya nyani au mpox ikianza kutolewa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mwishoni mwa wiki, mhudumu wa kwanza kupokea chanjo hiyo amesema msingi mkuu ni kuhakikisha analinda wale anaowahudumia.
Muyisa Kalala Raymond, Daktari kutoka hospitali Kuu ya Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini amesema alipata hamasa “kwa sababu sisi waganga tulitakiwa kupata chanjo ili virusi visienee katika jamii. Naamini chanjo ni nguzo mojawapo ya kujikinga na ugonjwa kwa sababu kwa kuchanjwa nikujikinga pia na jamii inayotuzunguka.”
Alimweleza George Musubao, mwandishi wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa aliyeshuhudia tukio hilo ya kwamba ni muhimu pia kwa wananchi kutoogopa chanjo dhidi ya mpox.
Chini ya usimamizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, chanjo ilizinduliwa katika mji wa Goma, mashariki mwa DRC Jumamosi Oktoba 5, 2024 ikilenga wahudumu wa afya na watoa huduma walio mstari wa mbele.
Mhudumu wa afya wa msalaba mwekundu akiwa mstari wa mbele kutokea akipatiwa chanjo dhidi ya MPOX. Mpango wa chanjo utaendelea kwa mda wa siku 10 jimboni Kivu Kaskazini, hadi Oktoba 16.
Walengwa wa chanjo na maeneo husika
Mathalani waliokutana na wagonjwa wa mpox na piwa waliokuwa wameambatana nao kwa njia moja au nyingine. Chanjo itatolewa katika maeneo 11 ya yaliyoathirika zaidi katika majimbo ya Equateur, Kivu Kaskazini, Sankuru, Kivu Kusini, Ubangi Kusini na Tshopo, ilisema WHO Afrika katika taarifa kwa vyombo vya habari.
DRC imepokea dozi 265,000 za chanjo ya mpox iliyotolewa na Mamlaka ya Utayarishaji wa Dharura ya Kiafya ya Tume ya Ulaya na Serikali ya Marekani. Daktari Muhamed Bashir msimamizi ya mpango wa mapambano ya WHO dhidi ya mpox nchini DRC anazungumzia umuhimu wa chanjo na msaada muhimu wa WHO kwa DRC katika janga hili akisema, "WHO inaunga mkono serikali ya DRC katika masuala ya afya na hasa katika eneo la kukabiliana na mpox tuko katika sekta zote za msaada na hasa leo katika uzinduzi wa kampeni ya chanjo dhidi ya mpox, chanjo hii ambayo ni muhimu sana katika vita dhidi ya maambukizi na mzunguko wa virusi katika Kivu Kaskazini. Kwa hivyo tunaunga mkono serikali katika ngazi ya kitaifa, katika ngazi ya mtaa na mkoa katika mapambano haya. “
Ametaja hatua nyingine muhimu kuwa ni maabara ya uchunguzi, utoaji taarifa muhimu, kutambua idadi ya wagonjwa na vile vile kuhudumia wagonjwa. Tayari ujumbe wa WHO kutoka Kinshasa, mji mkuu wa DRC unatembelea vitu vya matibabu kwenye majimbo yaliyoathirika zaidi.
UNICEF na usaidizi wa dawa za tiba
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF halikusalia nyuma kwa kutambua madhara ya mpox kwa watoto. Msaada wa dawa ulikabidhiwa kwa Naibu Gavana wa jimbo la Kivu Kaskazini.
Mariam Sylla, Naibu Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC anasema, “ni msaada wa tani 80 ambao ni dawa za kutibu MPOX. Kama mnavyojua MPOX inaathiri sana watoto katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, karibu asilimia 60 ya wagonjwa ni watoto wenye umri wa chini ya miaka kumi na tano. Kwa hiyo kwa UNICEF ni kero kubwa, tumehamasishwa kutoa msaada kwa serikali ya DRC hasa katika maeneo ya kipaumbele, hasa hapa Kivu Kaskazini. Dawa hizo zitapelekwa pia kwa majimbo mengine, Ituri na Kivu Kusini".