Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Peter Serukamba ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kuanza rasmi utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye Vitongoji (HAMLET ELECTRIFICATION PROJECT II) kwenye vitongoji 105 vya majimbo saba (7) ya mkoa wa Iringa ambapo Wateja 3,465 wataunganishiwa huduma ya umeme.
Akizungumza na Wanahabari ofisini kwake, leo wakati wa zoezi la kumtambulisha Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo katika mkoa wa huo, kampuni ya STEG International Services kutoka Tunisia; Mhe. Serukamba amesema kwa Serikali imedhamilia kuwaletea Watanzania maendeleo kwa kuwa nishati ya umeme ni moja ya nyenzo za kuwainua watu kiuchumi na kijamii.
“Tunashukuru, vijiji vyote 360 vya mkoa wa Iringa vina umeme, tuna kila sababu ya kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita; inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufikisha huduma ya umeme kwenye mkoa wetu wa Iringa; na sasa tunaamia kwenye vitongoji, nawapongeza REA na TANESCO kwa kazi kubwa ya kufikisha umeme kwa Wananchi wa mkoa wetu.” Amekaririwa Mhe. Serukamba.
Mhe. Serukamba ameipongeza REA kwa kuwasimamia Wakandarasi wanaosambaza huduma ya umeme kwa Watanzania na ametoa wito wa kuendelea, kuwasimamia ili wamalize Miradi ya nishati vijijini kwa wakati.
Viongozi wa REA; wakiongozwa na Msimamizi wa Miradi Nyanda za Juu Kusini, Mhadisi, Dunstan Kalugira wamemwambia Mkuu wa mkoa wa Iribga kuwa kazi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji 105 vya mkoa huo ilianza rasmi tarehe 20 Agosti, 2024 baada ya REA kwa niaba ya Serikali kusaini mikataba na Wakandarasi kwa lengo la kusambaza umeme kwenye vitongoji zaidi ya 3,000 kote nchi ambapo kupitia Mradi huo, mkoa wa Iringa umenufaika kwa kupata vitongji 105 ambavyo ni vitongoji 15 kwa kila Jimbo la uchaguzi kwa mkoa wa Iringa.
Majimbo hayo ni pamoja na Isimani; Iringa Mjini; Kalenga; Kilolo; Mafinga; Mufindi Kaskazini na Mufindi Kusini.
Katika taarifa yake ya awali, Mhandisi, Kalugira amemwambia Mkuu wa mkoa wa Iringa kuwa Mradi huo, utahusisha ujenzi wa umeme wa msongo mdogo wa kilomita 210; msongo wa kati wa kilomita 40.7; kuunganisha Wateja wa njia moja 3,150 na kuunganisha Wateja wa njia tatu 315.
Alisema REA inatekeleza Miradi kwa kushirikiana na Viongozi wa maeneo husika na kwamba utambuzi wa vitongoji hivyo vya Mradi ulifanywa kwa kushirikisha Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo yote saba ya mkoani wa Iringa.
Naye Bwana Aymen Louhaichi; Meneja wa STEG International Services nchini amesema kampuni yao itaukamilisha Mradi kwa mujibu wa mkataba na kwamba maandalizi yote muhimu yameshaanza.