ACT- Wazalendo yalia na serikali tatu

8 months ago 1007

Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Shangwe Ayo.

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema katika kuelekea sherehe za miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, kinataka muundo wa serikali tatu ili serikali ya Mapinduzi Zanzibar iwe na mamlaka kamili.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Shangwe Ayo wakati akizungumza na waandishi wa habari.

"Tunatambua kwamba kilio cha Wazanzibar ni kuwa na mamlaka kamili. Na sisi ACT-Wazalendo tutakuwa sehemu ya kuhakikisha Wazanzibar wanapata mamlaka hayo kamili," amesema Shangwe.

"Kinachohitajika ili kukamilisha yote haya Katiba mpya inahitajika na tumepiga kelele kuihitaji...na tunaihitaji tangu jana na si leo tu...hii ndio itatupatia muundo wa serikali tatu, serikali ya Tanganyika na serikali kamili ya Zanzibar halafu kwenye Muungano ndio tutafute serikali ya kutuunganisha."

Amesema kaulimbiu ya maadhimisho hayo itajulikana kama miaka 10 ya kupigania maslahi ya wote na Zanzibar yenye mamlaka kamili ambayo inaakisi ahadi yao kwa Watanzania ya taifa la wote, maslahi ya wote.

"Na ahadi yetu kwa Wazanzibari ni Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili," amesema Shangwe.

Kadhalika, amesema kilele cha maadhimisho ya kuanzishwa kwa chama hicho itakuwa Mei 5, mwaka huu na kwamba kabla ya hapo watafanya shughuli mbalimbali ikiwamo za kijamii na kutoa misaada ya kibinadamu kwa wagonjwa na walioathirika na mafuriko.

Amesema mambo mengine ambayo wanatarajia kufanya katika kuadhimisha miaka 10 ni kongamano la vijana ambalo linatarajiwa kufanyika Zanzibar April 21, mwaka huu likilenga kujadili dhima na wajibu wa kundi hilo katika kupigania Zanzibar yenye mamlaka kamili.

Pia wanatarajia kufanya mkutano wa kidemokrasia Moshi mkoani Kilimanjaro Aprili 27 mwaka huu na kuzindua nembo na bendera mpya.

"Pamoja na ushiriki huu wa mikutano na makongamano, wanachana watashiriki shughuli mbalimbali za kijamii kama vile kuchangia damu, kufanya usafi kwenye hospitali na kuwafariji wagonjwa,"amesema Shangwe.

"Mkesha wa ACT-Wazalendo utakuwa Mei 4, mwaka huu Makao Makuu Dar es Salaam na Ofisi Kuu ya chama Zanzibar, mkesha huu utashuhudia kupandishwa kwa bendera mpya za chama na Mei 5 itakuwa ni kilele na sherehe za maadhimisho haya na zitafanyika mkoani Kigoma na Mwenyekiti wa chama, Othman Masoud Othman, atahutubia taifa."

Chamahicho kimetoa rai kwa wanachama wake wote na viongozi nchi nzima, mikoa yote Tanzania kushiriki maadhimisho hayo ya miaka 10 ya kuzaliwa kwa chama hicho chetu kwa kufanya shughuli za kijamii na kupandisha bendera kwenye ofisi zetu zote. 

“Tunatoa shime kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wa chama kushiriki nasi kusherehekea miaka 10 ya mafanikio makubwa katika ujenzi wa demokrasia ya vyama vingi hapa Tanzania.”

Source : Kimataifa

SHARE THIS POST