AbalKassim apotezea ushindi wa TZ Prisons

3 months ago 44

By  Victoria Melkiad

Mwananchi Communications Limited

FOUNTAIN Gate juzi ilipoteza mechi ugenini mbele ya Tanzania Prisons iliyowanyoa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, lakini kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Abalkassim Suleiman amesema hakuna walichowazidiwa na wenyeji wao licha ya kupoteza pambano hilo.
Hilo lilikuwa pambano la pili kwa Fountain kupoteza ugenini baada ya awali kuchapwa mabao 4-0 na Simba, huku ikiwa imefunga mabao 14 na kufungwa 12 ikikusanya pointi 13 katika mechi saba ilizocheza hadi sasa, hata hivyo AbalKassim alisema wenyeji walikuwa na bahati na wala hawakuwazidi uwanjani.
Akizungumza na Mwanaspoti kiungo huyp wa zamani wa Ruvu Shooting ambaye amesajiliwa msimu huu katika klabu hiyo alisema kuwa, mchezo haukuwa upande wao ndiyo maana timu ilifungwa.
Alisema kuwa mchezo huo ulimalizika, lakini mioyo yao kama wachezaji hawakufurahishwa na matokeo waliyopata.
“Hatuwezi kushinda kila siku, ila kuna mechi nyingine unaona kabisa nafasi ya kushinda iko upande wako lakini mwisho haiwi hivyo.
“Tutaendelea kufanya vizuri kwani mchezo umekwishamalizika japokuwa inaumiza, lakini hakuna namna,” alisema Abalkassim, aliyefunga bao la pili la timu hiyo  baada ya awali Seleman Mwalimu kuitanguliza kwa bao la mapema lililosawazishwa na Ezekia Mwashilindi kwa mpira wa friikiki.
Fountain itakuwa nyumbani Oktoba 20 dhidi ya KMC, ikiwa na rekodi ya kufungwa bao 1-0 katika mechi mbili zilizocheza msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara.

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST