40 Gofu nchi 9 kuliamsha Zanzibar

3 months ago 84

WACHEZA gofu 40 kutoka mataifa 9 duniani wamethibitisha kushiriki katika michuano ya maalum ya Maofisa Watendaji Wakuu na Mabalozi, huku waandaaji wake wakisema zimesalia nafasi 30 tu kabla ya mashindano kutimua nyasi visiwani Zanzibar mwezi Septemba mwaka huu.

Nahodha wa Klabu ya Gofu ya Sea Cliff ya Zanzibar na mratibu wa mashindano hayo, Elias Soka alisema jana kuwa ni wachezaji 70 tu ndiyo wanatakiwa kushiriki katika mashindano ya mwaka huu.

Mashindano haya siku moja yatapigwa katika mashimo 18 kwenye viwanja vya Sea Cliff vilivyopo katika fukwe za Mangapwani visiwani Zanzibar mwanzoni mwa  mwezi Septemba, kwa mujibu wa Soka.

Akiendelea alisema: "Rasmi mashindano haya yanajulikana kama Faraja ya Burudani kwa Maafisa Watendaji Wakuu wa Kampuni na Taasisi mbalimbali  pamoja na maafisa kutoka balozi mbalimbali zilipo ndani na nje ya nchi, ndiyo maana hadi sasa tumeweza kusajili zaidi ya washiriki 40 kutoka mataifa tisa."

Kwa mujibu wa mratibu Soka, mashindano haya ni sehemu ya kampeni ya Tanzania kuboresha utalii kwa kutumia michezo kama gofu.

Wakati kukiwa na idadi hiyo ya washiriki majuma matano kabla ya mashindano kuanza, Soka alisema kumekuwepo pia na ongezekeo la idadi ya wadhamini wa michuano hii, hali ambayo amedai itasaidia pia kuboresha ukubwa wa zawadi za washindi watakaoshinda michuano hii.

Baadhi ya wadhamini wapya wa mashindano ya mwaka huu ni pamoja na Nathan Digital, Tanzanite Museum na Auric Air.

"Hii itasaidia pia kuvitangaza viwanja vya Sea Cliff kama moja ya viwanja bora vya mashimo 9 vilivyopo katika bahari ya Hindi," aliendelea.

GofU maalum kwa maafisa watendaji wakuu na wafanyakazi wa balozi mbalimbali  hufanyika kila mwaka visiwani Zanbzibar na washiriki wake wengi hutoka pembe zote za bara la Afrika na nje ya bara hili kwa mujibu wa Soka.

Wadhamini ambao wamekuwa wakifanikisha mashindano haya kwa kipindi cha miaka mitatu sasa ni pamoja na TBL, Exim Bank, Max Insurance, Phoenix Insurance, Melia Zanzibar, Zanzi Resort na waandaaji wake Sea Cliff Hotel ya Zanzibar.

Kilichoongezeka pia katika mashindano ya mwaka huu ni divisheni ya wanawake kwa ajili ya kutoa hamasa kwa wanawake ili washiriki kwa wingi katika mchezo wa gofu.

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST